AUAWA KWA KUPIGWA MAWE BAADA YA KUIBA KUKU MWANZA


MTU mmoja ameuawa na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa kosa la wizi wa kuku watano wilayani Kwimba mkoani Mwanza.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema Agosti 21, mwaka huu saa tatu kasoro robo asubuhi katika kitongoji cha Busulwa, Kata ya Ngulla Wilaya ya Kwimba, Leonard Mathias (23), mkazi wa Kijiji cha Ngulla, aliuawa na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi.

Kamanda Msangi alisema watu hao walimpiga kwa fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumchoma moto hadi kupoteza maisha kwa kosa la wizi wa kuku watano mali ya Ester Robert ambaye ni mkazi wa kijiji hicho cha Ngulla.

Alisema, “Inasemekana kuwa mtu huyo aliiba kuku watano nyumbani kwa Ester Robert kasha akakimbilia kijiji cha jirani cha Mwabomba. Inadaiwa kuwa wananchi wa kijiji cha Mwabomba walipomuona akiwa na kuku hao walipata mashaka kisha walimkamata na baadaye walitoa taarifa Kijiji cha Ngulla ndipo mwenye kuku alifika na kukabidhiwa kuku wake.

“Inadaiwa kuwa baada ya marehemu kukabidhi kuku kwa mwenye mali, wananchi walimchukua na kwenda naye kituo cha polisi, lakini wakiwa njiani walianza kumshambulia kwa kumpiga fimbo na mawe sehemu mbalimbali za mwili wake na baadaye kumchoma moto.

Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema ndipo walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo na tukio na kufanikiwa kukamata watu saba ambao wanadaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika mauaji hayo,” alieleza kamanda huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527