HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA ZAINAB TELACK KWENYE KIKAO CHAKE NA WAWEKEZAJI NA WAFANYABIASHARA WA MKOA WA SHINYANGA
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akizungumza na wafanyabiashara na wawekezaji mkoa wa Shinyanga leo Alhamis Julai 20,2017-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog


HOTUBA YA MHE. ZAINAB R. TELACK, MKUU WA MKOA WA SHINYANGA KWENYE KIKAO  CHAKE PAMOJA NA WAFANYABIASHARA WA MKOA WA SHINYANGA TAREHE 20/07/2017.

Mwenyekiti wa TCCIA,
Katibu Tawala Mkoa,
Wahe. Wakuu wa Wilaya,
Wakuu wa Sehemu na Vitengo, Sekretarieti ya Mkoa,
Wakurugenzi na Mameneja wa Mamlaka na Taasisi za Serikali,
Wawekezaji na Wafanya Biashara,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Habari za asubuhi.

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema wake kuendelea kutulinda, hatimaye kuweza kukutana siku ya leo.

Ndugu washiriki
Nimewaiteni kwa nia ya kuja kuwafahamisha umuhimu wenu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla, kuwaomba tudumishe mahusiano kati yetu – Serikali na ninyi Sekta Binafsi  ili kila upande uweze kunufaika kama ilivyokusudiwa.

Lakini pia nimewaiteni ili niweze kuwafamisha kuwa huu ni mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/2021) wenye dhima ya ‘‘Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Maendeleo ya Watu’’.

Ili kutimiza malengo ya Mpango huu ni lazima Serikali ifanye kazi kwa ushirikiano wa karibu sana na Sekta Binafsi, na ninyi ni sehemu ya Sekta Binafsi.  Ili kudumisha ushirikiano huo Serikali imeanzisha Mabaraza ya Biashara katika ngazi za Taifa, Mikoa na Wilaya.

Mabaraza haya yanaundwa jumla ya wajimbe  40 kwa uwiano sawa kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, yaani wajumbe 20 kutoka Sekta ya Umma na wajumbe 20 kutoka Sekta Binafsi.

Na baadhi yenu ni wajumbe wa mabaraza haya. Madhumini ya mabaraza  haya ni kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji, kuibua fursa za uwekezaji na kuzinadi fursa hizo kupitia vikao, mikutano, makongamano, majukwaa na midahalo ya uwekezaji.

Nitumie fursa hii kuwasihi wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa mliopo sasa na mtakaoteuliwa kwa nyakati za baadaye kushiriki kikamilifu vikao, mikutano, makongamano, majukwaa na midahalo ya uwekezaji kila mnapohitajika, ili muweze kutumia vizuri nafasi mliyopewa; kwani mmepewa dhamana ya kuwakilisha kundi kubwa la wawekezaji na wafanyabiashara wenzenu.

Napenda kutumia fursa hii kuwaandaa kwa ajili ya kushiriki kwenye Jukwaa la Uwekezaji litakalofanyika hivi karibuni katika Mkoa wetu; kupitia Jukwaa hilo Mkoa utapata nafasi ya kutangaza fursa zake za uwekezaji kwa wadau walio ndani na nje ya nchi. 

Lakini pia wafanya biashara na wenye viwanda watapata nafasi ya kutangaza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Ndugu washiriki
Uwekezaji ni moja ya shughuli zinazochochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla. Hadi sasa Mkoa una jumla ya viwanda 81; ambapo viwanda vikubwa ni 18, viwanda vya kati ni 9 na viwanda vidogo ni 54.

Napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza wafanya biashara na wawekezaji wote kutoka ndani na nje ya nchi kwa mchango wenu mkubwa katika uwekezaji, utoaji wa ajira kupitia biashara na viwanda vyenu na mchango wenu katika ukuaji wa uchumi na mapato ya ndani kupitia malipo ya kodi. 

Ikumbukwe kuwa kwa sehemu kubwa   jukumu la uwekezaji linatekelezwa na sekta binafsi; kazi ya Serikali ni kuandaa mazingira rafiki kwa ajili ya wawekezaji kama vile kudumisha amani na utulivu, kuweka miundombinu ya maji, barabara,  reli, umeme wenye uhakika na upatikanaji wa nishati mbadala kwa gharama nafuu. 

Kazi nyingine ya Serikali ni kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji na upatikanaji endelevu wa malighafi inayohitajika kwenye viwanda. Vitu hivi vikikosekana hakuna uwekezaji utakaofanikiwa kwa namna yoyote mahali popote. 

Ndugu Washiriki
Mkoa wa Shinyanga umetenga jumla ya Hekta 22,099.12 kwa ajili ya uwekezaji wa miundombinu ya biashara, kilimo na viwanda kama ifuatavyo:- Halmashauri ya Mji wa Kahama imetenga Hekta 2,000, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Hekta 5,560, Ushetu Hekta 2,110, Kishapu Hekta 10,361.70, Manispaa  ya Shinyanga Hekta 1,809.87 na  Msalala Hekta. 257.53.

Kufuatia uhamasishaji unaoendelea kufanywa na Mkoa, viwanda vingi vya kuchakata mazao ya kilimo na vimeanzishwa na kusababisha mahitaji makubwa ya malighafi kama vile pamba, mbegu za alizeti, matunda ya maembe na mapera, maharage ya soya, mpunga pamoja na pumba zake.

 Kufuatia hali, naomba kutumia fursa hii kuwahamasisha kuwekeza katika kilimo cha kisasa cha umwagiliaji kwa lengo la kupata mavuno yatakayotosheleza mahitaji ya viwanda vyetu; kwani soko la mazao mtakayozalisha ni la uhakika kutokana na uwepo wa viwanda vya kuchakata malighafi husika. 

Fursa zingine za uwekezaji katika Mkoa wetu ni pamoja na ujenzi wa viwanda vya nguo, nyama, ngozi na bidhaa zake. Fursa zingine ni kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani madini ya dhahabu. 

Ndugu washiriki
Suala la hifadhi ya  mazingira ni muhumi kwa nchi yoyote yenye maono endelevu ya kuimarisha sekta ya viwanda na ustawi wa jamii  yake. 

Viwanda vinapoendeshwa bila kuzingatia hifadhi ya mazingira vinakuwa ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira, hali inayopelekea athari mbalimbali katika jamii kama vile milipuko ya magonjwa, mabadiliko ya tabia nchi, ukame, kuongezeka kwa joto kwenye uso wa Dunia na  mvua kubwa kupita kiasi inayopelekea kutokea kwa mafuriko.

Serikali inatambua hilo na ndiyo maana katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika Kimkoa Wilayani Kishapu mwaka huu Kaulimbiu ilikuwa ‘‘Hifadhi ya Mazingira Mhimili kwa Tanzania ya Viwanda’’.

Mazingira ya Mkoa wa Shinyanga yamekuwa  kivutio kikubwa cha wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi. 

Viwanda vikubwa vimekuwa vikijengwa Mkoani tangu kukamilika kwa mradi mkubwa wa  maji ya Ziwa Victoria, uwepo wa umeme wa gridi ya Taifa, usafiri kwa njia ya reli na barabara ya lami inayounganisha Mkoa wa Shinyanga na Majiji makubwa ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam pamoja na  nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, vimekuwa ni vivutio vikubwa vya uwekezaji.

Ndugu washiriki
Suala la kupata taarifa sahihi ni muhimu sana kama tunataka kuendesha shughuli zetu kwa ufanisi. 

Taarifa zinapatikana kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na kupitia vyombo vya habari, mikutano na mitandao. 

Njia ya kupata taarifa kwa njia ya mikutano ni moja ya njia madhubuti kwani unapata muda wa kubadilishana mawazo na uzoefu ana kwa ana, unapata muda wa kuuliza na kujibiwa maswali yako kwa uhuru zaidi; ndiyo maana leo tumeweza kuitana mbali na kufahamiana, lakini pia tutaweza kubadilishana uzoefu katika uendeshaji wa biashara, pamoja na kujadili namna ya kutatua changamoto zinazotukabili kwenye biashara zetu.

Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa mara nyingine kwa kuitikia wito huu, kwani kikao hiki ni dalili nzuri ya ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi.

 Mikutano kama hii ni muhimu kwani tunapata nafasi ya kupeana taarifa muhimu kama vile fursa za uwekezaji zilizopo, upatikanaji wa masoko ya bidhaa zetu na mbinu endelevu za kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu; yote haya ni kwa nia ya kuhakikisha kuwa tunafikia malengo ya taasisi zetu na Taifa kwa ujumla.

Baada ya maelezo haya, napenda kutamka kuwa kikao hiki cha Wafanya Biashara wa Mkoa wa Shinyanga, kimefunguliwa Rasmi leo Tarehe 20 Julai, 2017.
Nawatakieni kikao chema na majadiliano yenye mafanikio.

Asanteni kwa kunisikiliza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post