USHAHIDI WA BABA MZAZI WASABABISHA AHUKUMIWE KUNYONGWA KWA KUMUUA BABU YAKE HUKO MBEYA

Mahakama Kuu kanda ya Mbeya, kwa kusaidiwa na ushahidi wa baba mzazi wa mshitakiwa, imemhukumu kunyongwa hadi kufa, Geoffrey Sichizya (27) baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumua babu yake ili achukue ng’ombe wake tisa.


Akisoma hukumu hiyo kwenye Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana, Jaji wa Mahakama Kuu Atuganile Ngwala alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili ameridhika pasipo kuacha shaka kuwa mshitakiwa alimuua babu yake Labson Sichizya kwa kukusudia.


Alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa na Meas Sichezya ambaye ni baba mzazi wa mshitakiwa huyo, pamoja na Mashaka Sichizya ambaye ni ndugu wa damu, ambao kwa pamoja walimkamata siku ya tukio wakiwa na viongozi wa vijiji na kumpeleka polisi.


Jaji Ngwala alisema Geofrey kwenye maelezo yake kwa mlinzi wa amani alidai kuwa alimuua babu yake ili achukue ng’ombe tisa waliokuwa wanamilikiwa na babu huyo.


Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga kwamba mshitakiwa alimkaba koo babu yake Sichizya hadi kufa Novemba 19, 2012 saa 2:00 asubuhi katika kijiji cha Sakamwela, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.


Aliendelea kusema kuwa mshitakiwa huyo baada ya kumuua babu yake huyo kwa kumkaba koo na kufariki, alimfunga na kamba ya chandarua shingoni na kumning’niza kwenye mti nyuma ya nyumba yake ili ionekane kama marehemu alijinyonga.


Mshitakiwa huyo alikuwa akitetewa na wakili Kamru Habibu, ambaye baada ya hukumu kutolewa hakuwa na hoja yoyote mbele ya mahakama hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post