MAJAMBAZI YALIYOUA ASKARI POLISI 8 TANZANIA YAUAWA

Jeshi la Polisi Tanzania limesema limewaua majambazi wanne ambao walikuwa ni sehemu ya kundi la majambazi lililowashambulia na kuwaua askari 8 wilayani Kibiti mkoani Pwana jana usiku.


Akizungumza na wanahabari leo, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Nsato Marijani amesema kuwa mara baada ya kundi hilo kuwashambulia askari, kikosi kingine cha askari kilifanya msako na kubaini maficho ya majambazi hao.


Amesema baada ya kuwabaini, yalifanyika mashambulizi ya kurushiana risasi, ambapo majambazi wanne waliuawa pamoja na kukamata bunduki 4 zikiwemo SMG mbili zilibainika kuwa kati ya zile zilizoporwa na majambazi hao.


Akielezea tukio hilo lilivyokuwa, Kamishna Marijani amesema kundi la waharifu walikuwa na silaha za moto na ambao idadi yao haikujulikana liliweka mtego na kufanikiwa kuishambulia kwa risasi gari iliyokuwa na askari 9 waliokuwa wakitoka katika malindo kurudi kambini, na kuwaua askari 8 kati yao huku mmoja akijeruhiwa mkononi.


Amewataja askari waliuawa kuwa ni pamoja na Mkaguzi Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub, ambapo pia walipora bunduki 7 zikiwemo SMG 4.


Kufuatia tukio hilo, Kamishna Marijani ametangaza vita na waharifu wote katika maeneo hayo, ambapo amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaanza oparesheni maalum katika mkoa wa Pwani, kuhakikisha vinawasaka na kukomesha mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua.


"Mpaka sasa jeshi limekwisha poteza skari zaidi ya 10, inatosha…. Tunakwenda kwenye oparesheni maalum, hatutakuwa na mzaha, tutawasaka popote walipo na kuwashughulikia kikamilifu, ,,, watajua tofauti ya moto na maji… mpaka jana idadi ilikuwa ni 8 kwa nne, lakini nawahakikishia kuwa ndani ya wiki moja idadi hiyo itakuwa imebadilika, na tutakuwa na hesabu tofati” amesema Marijani


Kuhusu hofu ya ugaidi, Kamishna Marijani amesema tukio hilo siyo la kigaidi bali ni uhalifu wa kawaida, huku akibainisha kuwa Tanzania hakuna ugaidi


Katika hatua nyingine, jeshi hilo limepiga marufuku uendeshaji wa pikipiki katika maeneo yote ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji zaidi ya saa 12:00 jioni. Amesema usafiri wa boda boda utaruhusiwa kati ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post