MWENYEKITI WA KITONGOJI AUAWA KWA KUPIGWA RISASI



Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Boniventure Mushongi,anayehamia mkoa wa Simiyu akizungumzia tukio la mauaji ya mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo huko Rufiji (Picha na Mwamvua Mwinyi)


MAUAJI kwa viongozi wa vijiji na vitongoji mkoani Pwani hususan wilayani Rufiji vimeendelea kujitokeza ambapo mwenyekiti wa kitongoji cha Kazamoyo wilayani Rufiji Hemed Njiwa (45) ameuawa kwa kupigwa risasi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi ambaye anahamishiwa mkoa wa Simiyu alisema marehemu aliuawa na watu wasiojulikana wakati akiwa nyumbani.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia machi 13 ,eneo la Kifuru kata na tarafa ya Ikwiriri wilayani hapo.

“Marehemu alipigwa risasi kifuani akiwa nyumbani kwa mke wake mdogo Maimuna Abdallah (36)na alikutwa na jeraha la risasi kwenye mkono wake wa kushoto”,alisema.


Kamanda Mushongi,alieleza kwamba mtu ama watu aliyehusika na tukio hilo baada ya kumuua alikimbia kusikojulikana kwa kutumia pikipiki aina ya boxer ambayo haikuwa na namba za usajili.

Alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa na jeshi la polisi linaendelea na msako mkali ili kuweza kubaini watu waliohusika na tukio hilo.

Kamanda huyo aliwataka wananchi kuwafichua watu wanaohusika na matukio ya kuua viongozi wa vijiji na vitongoji kwani hilo linaweka idadi ya matukio zaidi ya matatu yaliyohusisha viongozi hao.
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post