WATANZANIA 132 WATIMULIWA NCHINI MSUMBIJI


SERIKALI imesema Watanzania 132 waliokuwa wakiishi nchini Msumbiji katika mji wa Monte Puez, Jimbo la Cabo Delgado wamerudishwa nchini kutokana na operesheni maalumu ya kuwakamata na kuwarudisha raia wa kigeni wanaoishi katika mji huo bila kufuata sheria za uhamiaji za nchi hiyo.

Operesheni hiyo inawakumba pia raia wa nchi nyingine waliomo katika mji huo wanaoishi nchini humo bila kufuata sheria za uhamiaji za nchi hiyo; na kwa Tanzania idadi hiyo inaweza kuongezeka.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Suzan Kolimba alisema hayo jana jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa tayari serikali imearifiwa kuwa operesheni hiyo imeanzia katika mji huo, kwa kuwa una raia wengi wa kigeni ikilinganishwa na miji mingine.

“Tumepokea taarifa za kukamatwa na kufukuzwa kwa raia wa Tanzania waliokuwa wakiishi katika mji wa Monte Puez, ulio umbali wa kilometa 1,000 kutoka Maputo (mji mkuu) katika Jamhuri ya Msumbiji,” alisema Dk Kolimba na kuongeza kuwa sio Watanzania pekee waliofukuzwa katika mji huo, bali hata raia wengine wa kigeni.

Alisema operesheni hiyo ilipoanza Februari 11, walirejeshwa raia 58 kupitia mkoani Mtwara, na ilipofika juzi wakarejeshwa wengine 24 na jana walirudishwa raia 50, huku akisema idadi hiyo inaweza kubadilika muda wowote.

Alisema kutokana na operesheni hiyo, Ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji upo katika eneo la tukio ili kufuatilia suala hilo na kuona hali halisi huku wakifanya mawasiliano ya kidiplomasia na Serikali ya Msumbiji kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao.

Aidha, alisema ubalozi pia unashirikiana na Serikali ya Msumbiji kwa pamoja na Uhamiaji walioko mkoani Mtwara, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa ili kubaini yale yaliyokuwa yakisemwa katika mitandao kwamba raia hao wanapigwa na kunyang’anywa vitu kama ni kweli na kama ikibainika, nchi hizo zitajua la kufanya.

Naibu Waziri alisema katika mji huo wa Monte Puez inakadiriwa wapo Watanzania wapatao 3,000 wanaoishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii na kwamba Tanzania hawatofautiani na operesheni hiyo, kwani wameingia kwa njia isiyo halali, lakini pia wakasihi watolewe kihalali na wakitendewa haki.

Dk Kolimba alisema serikali inawahakikishia Watanzania kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Msumbiji ni mzuri na mwaka jana nchi hizo zilifanya mkutano wa ujirani mwema uliolenga kuimarisha ushirikiano baina yao.

Hata hivyo, alitoa mwito kwa Watanzania wote waishio ughaibuni, kufuata sheria za taratibu za nchi hizo wanazoishi na watambue wanapokwenda nje ya nchi wahakikishe wanafuata taratibu, wakikumbuka pia hata Tanzania iliwahi kuendesha operesheni ya raia waliokuwa wakiishi nchini isivyokuwa kihalali nchini.

Tangu kuanza kwa operesheni hiyo, imedaiwa raia wa Tanzania waliokuwa wanaishi nchini Msumbiji wamefukuzwa na kurudishwa Tanzania, wakinyang’anywa mali zao, vitambulisho pamoja na hati za kusafiria na askari wa Msumbiji pasipo kujua sababu.

Aidha, katika ujumbe uliokuwa ukisambaa jana katika mitandao ya kijamii unaoaminika kutumwa na Watanzania hao imeeleza kuwa wameambiwa baada ya siku tano wawe wote wameondoka nchini humo.

“Sasa tunajiuliza kuna watu tuna biashara zetu za maduka zaidi ya moja na wengine nyumba zetu, tuna watoto huku na tumeonewa, tatizo ni nini, tatizo kuwa Mtanzania? Siku tano tutawezaje kuhamisha mali zetu? Tuna magari yanafanya biashara na mengine tunatembelea, ebu pazeni sauti ili serikali yetu isikie na iweze kutusaidia kabla ya siku tano tulizopewa kuanzia leo,” ulieleza ujumbe wa mmoja wa Watanzania walioko Msumbiji.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post