NAPE AWATAKA WAANDISHI WA HABARI KWENDA NA WAKATI...ZAMA ZIMEBADILIKA


SERIKALI imesema sekta ya habari inakabiliwa na changamoto katika uwasilishaji wa taarifa kwa umma kunakotokana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia hivyo kuwataka wadau kujitahidi kwenda na wakati hasa kwa upande wa redio ili wasipitwe na wakati.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye katika maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya habari nchini.

Alisema kuwa wakati umefika kwa wadau wa sekta ya habari kufikiri kwa kina namna ya kuhabarisha umma kwa kuangalia namna ya uwasilishaji ambapo kwa sasa changamoto kubwa ni kasi ya ukuaji wa teknolojia ya habari na namna ambapo redio zinaweza kushindana na vyombo vingine.

Alisema kwa wanahabari wanapaswa kuwa makini na taarifa wazitoazo kwa jamii kwani kumekuwa na mazoea ya baadhi yao kuripoti habari bila kufanya uchuinguzi wa kina huku wakitumia chanzo kimoja cha habari badala ya kujiuliza maswali mengi ili kupata taarifa sahihi.

Akizungumzia urasimu wa upatikanaiji wa habari mikoani, wilayani na wizarani alisema kuwa Sheria ya Habari imempa nguvu Mkurugenzi wa Habari Maelezo amabaye ndiye msemaji mkuu wa serikali awajibike kutoa habari za serikali.

Alisema kuwa kwa kipindi cha nyuma maofisa habari walikuwa hawahudhurii kwenye vikao muhimu vya maamuzi, hivyo kutokuwa na taarifa sahihi. Alisema kuwa kama waziri mwenye dhamana na wizara hiyo lengo la serikali ni kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi kwa ukuaji wa tasnia ya habari hata kama ni kwa kubadilisha sheria inayobana uhuru wa habari.

Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Vyombo vya Habari Jamii Tanzania-COMNETA, Prosper Kwizige alisema kuwa ipo changamoto kwa baadhi ya maafisa habari mikoani na wilayani kuleta urasimu mkubwa katika utoaji wa taarifa zinazohitajika kwa waandishi wa habari hivyo kukwamisha upatikanaji wa habri kwa umma.

Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Edefonce Nfuka alisema kuwa maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muafaka kwa wadau wa sekta hiyo kutoa mrejesho wa wahitimu kutoka kwenye vyuo hapa nchini na hivyo kusaidia katika uboreshaji wa mitaala ili kuwa na wahitimu mahiri kwenye sekta hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayubu Rioba alisema kuwa kwa siku za nyuma redio ilikuwa ni chombo cha kuaminika katika utoaji wa habari hivyo kujijengea umaarufu na kuaminika zaidi tofauti na ilivyo sasa ambapo kuna upotoshaji mkubwa.
Na Vincent Mpepo-OUT 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post