MWANAMKE AKAMATWA KWA DAWA ZA KULEVYA SHINYANGA,AKUTWA NA SHILINGI MILIONI 10.8 CHINI YA GODORO..TAZAMA PICHAKamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Muliro Jumanne Muliro
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro akionesha pesa kiasi cha shilingi milioni 10 na laki 8 za mtuhumiwa wa dawa za kulevya-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Muliro Jumanne Muliro
Mkoba ukiwa na fedha za mtuhumiwa wa dawa za kulevya
*****
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kukamata watuhumiwa 33 kutoka wilaya ya Shinyanga,Kahama na Kishapu kwa kosa la kujihusisha na usafirishaji,uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya aina ya Cocaine,Heroine,bangi na mirungi.

Miongoni mwa watuhumiwa hao yumo mwanamke aitwaye Ashura Ramadhan aliyekutwa na pesa taslimu shilingi Milioni 10 na laki 8 alizokuwa amezificha chini ya godoro chumbani kwake zinazodaiwa kuwa zinatokana na dawa za kulevya.

Akizungumza na vyombo vya habari jana kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro alisema watuhumiwa hao wamekamatwa wakati wa operesheni kali ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ya wiki mbili iliyoanza Januari 30,2017 ambayo wiki ya kwanza walijikita katika kuzifuatilia kwa siri za umakini wa hali ya juu taarifa zote za kiintelijensia zinazohusiana na dawa za kulevya.

Alisema baada ya kuzichuja vizuri taarifa hizo kwa lengo la kuepuka ubambikizaji wa kesi walifanya operesheni kwa vitendo kwa upekuzi na ukamataji wa watuhumiwa kuanzia Februari 6,2017.

“Tulikamata watuhumiwa 33,tulikamata gramu 480 za heroine na cocaine,bangi kilo 81,kete za bangi 1,370,misokoto 1,230 ya bangi,mirungi kilo 3 na gramu 1,027 pamoja na vifaa saidizi vya kujidungia dawa za kulevya ikiwemo sindano na bomba za sindano 8 zenye ujazo wa CC 0.5”,alieleza Muliro.

Alisema miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa ni Said Nassor Al-Mahrouqi (27) mwarabu mkazi wa Nyasubi wilayani Kahama na Muscat nchini Oman aliyekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na usafirishaji,usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya aina ya heroine.

Wengine waliokamatwa ni John Mathias(44) mkazi wa Nyasubi na Hassan Ahamad Sindimo(31) mkazi wa Nyihogo na wenzake wawili kwa kujihusisha na uuzaji na utumiaji wa mirungi.

Aidha jeshi hilo pia limemkamata mwanamke aliyejulikana kwa jina la Ashura Ramadhan (31) mke wa mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya ambaye tayari ameshafungwa jela kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya baada ya kumtuhumu akiendeleza biashara mme wake ya kuuza dawa za kulevya.

“Ashura anatuhumiwa kuendelea na biashara hiyo mkoani Shinyanga,na alipopekuliwa nyumbani kwake alikuwa na pesa taslimu Milioni 10.8 zikiwa zimefichwa chini ya godoro na upelelezi ukikamilika atapelekwa mahakamani na watuhumiwa wengine”,alieleza kamanda Muliro.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post