MUGABE: NIMEFURAHISHWA NA SERA ZA TRUMP...SIKUTAKA MADAM CLINTON ASHINDE


Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amesema anakubaliana na sera ya Rais wa Marekani Donald Trump kwamba "Marekani iwe ya Wamarekani".

Bw Mugabe, ambaye ndiye mara ya kwanza anazungumzia utawala wa Bw Trump, amesema alishangazwa na ushindi wa kiongozi huyo wa Republican.

Hata hivyo, amesema hakutaka pia "Madam Clinton ashinde", akirejelea mgombea wa chama cha Democratic aliyeshindwa uchaguzi wa Novemba mwaka jana Hillary Clinton.

"Lakini vilevile, ukija kwa Donald Trump ambapo anazungumzia uzalendo... Marekani iwe ya Wamarekani - katika hilo, nakubaliana naye. Zimbabwe iwe ya Wazimbabwe," Bw Mugabe amesema, kwenye dondoo ambazo zimechapishwa katika gazeti rasmi la serikali la Herald.

Ameongeza kwamba Bw Trump anafaa kupewa muda wa kudhihirisha uwezo wake.

"Sijui. Mpeni muda. Bw Trump huenda hata labda ataangalia upya vikwazo vilivyowekewa Zimbabwe," Bw Mugabe amesema.

Mahojiano kamili ya Bw Mugabe yanatarajiwa kupeperushwa rasmi kesho jioni kwenda sambamba na maadhimisho ya kusherehekea kiongozi huyo kutimiza miaka 93 tangu kuzaliwa kwake

Bw Mugabe pia amesema anafaa kuendelea kuongoza, kwani watu wengi nchini mwake wanahisi kwamba hakuna mtu anayetosha kuchukua pahala pake.

Kiongozi huyo tayari ameteuliwa na chama tawala cha Zanu-PF kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Bw Mugabe ameongoza Zimbabwe nchi hiyo tangu uhuru mwaka 1980.

Via>>BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post