MAMA AKATAA DHAMANA MAHAKAMANI AKITAKA ABAKI NA HOUSE GIRL WAKE RUMANDE

Mkazi wa Sitakishari Dar es Salaam, Christina Thomas (28), amekataa kudhaminiwa ili arudi rumande na msichana wake wa kazi ambaye alishindwa masharti ya dhamana.

Christina jana alifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa tuhuma za kumpiga mtoto wake wa miaka miwili na kumsababishia majeraha makubwa, kuzimia na kushindwa kumpeleka hospitalini.

Mwendesha Mashitaka Hilda Kato, alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ritha Tarimo kwamba mshitakiwa siku isiyofahamika Januari, alimpiga kwa fimbo mtoto huyo na kumsababishia majeraha.

Kato alidai katika mashitaka ya pili, mshitakiwa huyo ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo na msichana wake wa kazi, Blanka Benjamin kwa uzembe walimwacha mtoto huyo bila kumpeleka hospitali huku akiwa na hali mbaya ambayo ilisababishwa na mama mzazi.

Baada ya kusomewa mashitaka, mama huyo alijibu kuwa hakumbuki, huku mshitakiwa wa pili ambaye ni msichana wa kazi akikana mashitaka yake.

Mwendesha Mashitaka alimwambia Hakimu Tarimo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, lakini dhamana yao iko wazi kama watakidhi masharti. 

Hakimu alitoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika mmoja akiwa mtumishi kwenye taasisi inayofahamika na kusaini dhamana ya Sh 800,000 kila mmoja.

Baada ya kusomewa masharti hayo ya dhamana mshitakiwa namba moja alikidhi masharti ya dhamana huku wa pili akishindwa kutokana na wadhamini kuchelewa.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo wa kwanza ambaye ni mama wa mtoto alisema hawezi kuwa nje kwa dhamana akimwacha mshitakiwa wa pili rumande hivyo kumwomba hakimu warudi wote ndani hadi kesho watakapotimiza masharti ya dhamana pamoja.

Hakimu alimwambia mshitakiwa huyo kwamba kwa sababu yeye ana mtoto mdogo hivyo angeweza kutoka na kumwacha mshitakiwa wa pili na kesho (leo) angepata dhamana, lakini akasema mtoto wake ataondoka na baba yake, na yeye atarudi rumande hadi watakapopata dhamana wote wawili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post