WAZIRI MKUU AONYA VITA YA MADIWANI NA WATENDAJI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Idara kwenye Halmashauri za Wilaya na Manispaa wasaidie kutoa utaalamu badala ya kupingana na madiwani ili wawezeshe kuleta maendeleo kwa wananchi.

Pia amewataka madiwani wasikilize ushauri wa kitaalamu unaotolewa na Wakuu wa Idara katika utekelezaji wa miradi iliyotengwa na Halmashauri.

Ametoa wito huo jana mchana (Alhamisi, Januari 5, 2017) wakati akizungumza na watumishi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mabada na viongozi na watendaji wa mkoa wa Ruvuma akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani humo.

“Wakuu wa Idara nyie ni washauri. Tumieni taaluma zenu kutoa ushauri, semeni bila woga pale inapodidi. Ninawasihi waheshimiwa madiwani wasitumie fursa yao ya ‘kuazimia’ pale inapotokea kuna watumishi wenye msimamo,” alisema.

Akizungumzia kuhsu ukusanyaji wa mapato, Waziri Mkuu alisema Serikali iko makini kwenye matumizi kwa kila senti inayokusanywa na akawataka watumishi hao kila mmoja aongeze mapato ya Serikali kupitia sekta aliyopo. Pia amepiga marufuku matumizi holela ya fedha za umma.

“Kuanzia leo, marufuku kwa fedha iliyokusanya kwa mapato ya ndani kutumika bila utaratibu. Serikali hii haina mzaha na miradi inayotekelezwa chini ya viwango. Mtumishi ukiharibu hapa Madaba, usidhani utahamishwa, tunamalizana na wewe hapahapa. Wala usiombe ndugu yako akuombee uhamisho, tutakufuata hukohuko,”alisisitiza.

Aliwataka watumishi wa umma wote watumie Ilani ya Chaguzi ya CCM katika kutekeleza majukumu kwani inaeleza kila kitu ambacho Serikali inatakiwa kukifanya katika kipindi ca miaka mitano.

“Zaidi ya hayo, ninawasihi kila Mkurugenzi atoe nakala ya hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa Novemba 20, 2015 wakati akizindua Bunge la 11, awape watendaji wake waisome na kufanyia kazi maeneo yote aliyoyaainisha kwani ilitoa dira ya nini anataka kufanya katika Serikali hii,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Serikali kwa upande wake inaendelea kuboresha maslahi ya watumishi na imeanza kulipa madeni yaliyokuwa yamelimbikizwa. 

“Serikali imedhamiria kupunguza madeni ya watumishi na hadi kufikia Novemba 30, 2015 jumala ya sh. bilioni 28.9 zilikuwa zimekwishlipwa kwa watumishi 31,032 wenye madai katika sekta mbalimbali. Zoezi hili linaendelea.”

Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha watumishi wa wilaya hiyo wajibu wao wa kuwahudumia Watanzania bila kujali dini, itikadi, kabila au hali zao na akasisitiza kuwa Serikali haitamuonea mtumishi yeyote ambaye anatimiza wajibu wake.

Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.

"Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua kama hiyo hiyo, " alisema.

 IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post