WAUMINI KANISA LA ANGLIKANA NUSURA WACHAPANE MAKONDE

Baadhi ya waumini wa makanisa ya Anglikana   Dar es Salaam, nusura wazichape jana.

Hiyo ni baada ya mapadri wao kutaka kusoma waraka wa Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam unaomtetea Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk. Valentino Mokiwa, ambaye ametakiwa kujiuzulu kwa sababu ya kashfa mbalimbali.

Waraka huo uliokuwa unasomwa jana ulilenga kujibu  uliotolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini,  Dk. Jacob Chimeledya, ambao uliorodhesha tuhuma zilizokuwa zikimkabili Dk. Mokiwa ukisema kwa sasa dayosisi hiyo itakuwa chini ya Askofu Mkuu.

Baadhi ya makanisa ya Dar es Salaam, Januari 8, mwaka huu yalisomewa waraka huo wa Askofu Mkuu, Dk. Chimeledya huku mengine yakiwa hayajasomewa licha ya kutakiwa kufanya hivyo na ngazi ya taifa.

Jinsi ilivyokuwa
Katika baadhi ya makanisa, jana vurugu zilizuka mapadri walipoanza kusoma waraka wa Halmashauri ya Kudumu ya Dayosisi ya Dar es Salaam.

Hapo ndipo  baadhi ya waumini walipogoma wakisema wanataka kwanza kusomewa ule wa Askofu Mkuu wajue tuhuma zinazomkabili Dk. Mokiwa.

Katika Kanisa la Mtakatifu Batholomayo   Ubungo, hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya baadhi ya waumini   kupiga kelele na kwenda kumzimia kipaza sauti Padri wa Kanisa hilo, James Hiza, huku wengine wakinyanyuka kwenye viti wakimtaka  kutokuusoma waraka huo wa Mokiwa.

Kutokana na kelele hizo ndani ya kanisa,   mmoja wa waumini hao alikwenda kuzima mfumo wa umeme na kusababisha vipaza sauti kutofanya kazi.

Hata hivyo, hatua hiyo  haikusaidia kwa kuwa Padri huyo   alikuwa akiendelea kusoma waraka huo.

Kuona hivyo, baadhi ya waumini walisikika wakisema ‘kama unasoma huo hakikisha unasoma waraka zote mbili’.

Hapo Katibu wa Kamati Tendaji ya Kanisa, John Mapunda, alisimama akiwa ameshikilia waraka wa Askofu Mkuu nao  kumtaka ausome mbele ya waumini na kuuacha aliokuwa akiusoma.

Hata hivyo, Padri huyo aliendelea kusoma waraka aliokuwa nao na kutowajali waliokuwa wakimtaka kuacha kusoma waraka huo.

Mbali na katibu huyo wa kanisa, pia mzee wa makamo alikwenda kumsihi Padri huyo kutosoma waraka huo.

Lakini juhudi zao hazikuzaa matunda kwani alisoma waraka huo mpaka mwisho ingawa waumini waliendelea kupiga kelele muda wote bila kumsikiliza.

Baada ya kumaliza kusoma waraka huo Padri,  Hiza alirudi na kukaa katika nafasi yake  huku akiwataka waumini kutulia.

Waondoka na sadaka
Baada ya kumaliza kusoma waraka huo na vurugu kutulia, baadhi ya waumini ambao hawakuridhika na yaliyotokea walionekana kususa shughuli nyingine ikiwa ni pamoja na kutoa sadaka.

Waumini hao licha ya kuwa na bahasha maalumu ambazo hutumika kutolea sadaka, muda wa matoleo ulipofika, waliendela  kukaa kwenye viti vyao wakiwa na bahasha zao.

Pia wengine walisusa kushiriki Meza ya Bwana ingawa  wahudumu waliwasihi wasifanye hivyo.

“Tusimfanyie hasira Mungu, hata kama mmekasirika vumilieni tuendelee na ibada yaani hata kupokea mwili hamtaki?” aliwauliza  mhudumu wa kanisani humo.

Baada ya ibada, Katibu wa Kamati Tendaji,  Mapunda aliwaambia waandishi wa habari   kuwa  walikuwa wamefanya kikao na kukubaliana kutosoma waraka wowote kwa sababu Jumapili iliyopita hawakuusoma   ule uliotolewa na Askofu Mkuu. Dk. Chimeledya.

“Waraka wa Baba Askofu Chimeledya hakuusoma wiki iliyopita, alisema hajaupata kumbe ulikuwapo.

“Siku chache badaye na Askofu Mokiwa ambaye ameshafukuzwa katoa waraka wake.

“Huo ndiyo alitaka kuusoma tukamwambia kwa kuwa ule wa kwanza haukusomwa kanisani na huu usiusome au usome zote ili tusiingie katika mgogoro huu.  Alikubali lakini kafika madhabahuni akatugeuka,”alisema Mapunda.

Padri Hiza alipofuatwa na waandishi  kuzungumzia suala hilo alisema,“Hili suala limefikia ngazi ya juu  ya dayosisi, mimi siwezi kuliongelea kwa kuwa si msemaji wa dayosisi.”

Wakati hayo yakiendelea, polisi walikuwa wametanda  nje ya kanisa hilo.

Baada ya vurugu kutulia kanisani, polisi hao walionekena wakizungumza na Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Kanisa, Mapunda na baadaye wakaondoka kwenye eneo hilo.

Hali ya sintofahamu ilitokea pia katika Kanisa la Hollyghost Kimara Mbezi ambako mgogoro wa kutaka kusoma waraka wa Dk. Mokiwa au usisomwe, uliibuka na mwisho Padri akaamua kuacha kuusoma.

Kabla ya Padri kuacha kuusoma, zilizuka  vurugu za hapa na pale kiasi cha   watu kufikia hatua   ya kutaka kupigana.

Katika Kanisa la Mtakatifu Mariam Padre wa kanisa hilo alitaka kuusoma waraka wa Mokiwa lakini waumini walikuja juu na kuusoma wa Askofu Mkuu Dk. Chimeledya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post