WAFUNGWA WAMLALAMIKIA OFISA USTAWI WA JAMII KUENDEKEZA RUSHWA ADHABU MBADALA


WAFUNGWA katika Gereza la Kilimo la Songwe lililopo wilayani Mbeya mkoani Mbeya wamemlalamikia Ofisa Ustawi wa jamii wilayani Rungwe, kujihusisha na rushwa katika utoaji wa adhabu mbadala kwa wafungwa wanaokidhi vigezo vya kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha nje.

Wafungwa hao walisema Ofisa Ustawi huyo wa wilaya ambaye hawakumtaja jina lake amekuwa akipokea kati ya Sh 300,000 hadi 500,000 ili kuidhinisha mfungwa aliye na sifa kupewa adhabu mbadala ya kifungo cha nje.

Wafungwa wa gereza hilo walibainisha hayo juzi kwenye risala yao waliyoisoma mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliyotembelea gereza la Kilimo la Songwe ikiambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni.

Katika risala iliyosomwa na Mfungwa namba 246 wa mwaka 2016,George Albert,ilibainishwa kuwa mfumo huo wa matumizi ya rushwa umekuwa ukiwakosesha haki ya msingi ya adhabu mbadala wafungwa wasio na ndugu wenye uwezo wa kifedha.

Kutokana na hali hiyo, Albert aliiomba serikali kubadili mfumo wa kimamlaka katika usimamizi wa utoaji adhabu mbadala na ikiwezekana adhabu ya kifungo cha nje itolewe na mahakama iliyotoa hukumu husika au gereza alikofungwa mfungwa.

Mfungwa huyo pia aliiomba serikali kutenga majaji maalumu watakaokuwa kwa ajili ya kusikiliza rufani za hukumu ili kuwezesha kesi hizo kumalizika kwa wakati, tofauti na ilivyo sasa ambapo mfungwa anakaa gerezani na kutumikia kifungo muda mrefu kabla ya rufaa yake kuanza kusikilizwa, hatua inayowakatisha tamaa watu wengi.

Akizungumzia tuhuma za rushwa zilizobainishwa na wafungwa zikielekezwa kwa Ofisi ya Ustawi wa jamii wilaya ya Rungwe, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Masoud Ali aliitaka serikali kufuatilia kwa haraka jambo hilo na itakapobainika mhusika achukuliwe hatua stahiki.

Kwa upande wake Masauni alisema licha ya kuwa ofisi inayolalamikiwa haiko chini ya wizari yake, atahakikisha anawasiliana na waziri mwenye dhamana ili aweze kulishughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo.

Aliwataka wafungwa walio na vielelezo vinavyoweza kuthibitisha uwepo wa rushwa kwa ofisa anayelalamikiwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na iwe fundisho kwa maafisa wengine.
Via>>Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post