Video: SABABU ZA LOWASSA KUKAMATWA NA POLISI GEITA,WAANDISHI WA HABARI KUPIGWA


JESHI la Polisi Mkoa wa Geita, limemkamata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Lowassa ambaye pia alikuwa mgombea urais wakati wa uchaguzi mkuu mwaka juzi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amekamatwa mjini Geita jana muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Mkoa wa Kagera alikokuwa kwa shughuli za kisiasa.Mbali na Lowassa, viongozi wengine waliokamatwa ni Profesa Mwesigwa Baregu na Hamis Mgeja.

Lowassa na wenzake hao, walikuwa wakielekea Kata ya Nkome, Jimbo la Geita Vijijini kushiriki mkutano wa kampeni za udiwani.

Tukio hilo lilitokea jana saa 9:20 mchana baada mwanasiasa huyo kuwasili mjini Geita na kukuta wananchi wengi wakiwa wamejaa barabarani wakitaka awasalimie.

Kutokana na umati mkubwa wa watu waliokuwa barabarani, Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, yeye na msafara wake walilazimika kuingia eneo la stendi ya zamani ya mabasi kuwasalimia wananchi hao.

Hata hivyo, kabla hajaanza kuzungumza na wananchi hao, magari matatu yaliyokuwa yamejaa askari polisi yalifika mahali hapo na kumkamata.

Baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita na kukaa kwa dakika kadhaa, Lowassa na wenzake walihamishiwa ofisini kwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo kwa mahojiano.

MABOMU YA MACHOZI

Baada ya mwanasiasa huyo kukamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita, kundi la wananchi wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, walianza kueleka maeneo ya kituo hicho ili kujua kinachoendelea.

Wakati wakielekea katika eneo hilo, polisi walilazimika kuwatawanya kwa mabomu ya machozi yaliyoathiri wanafunzi wa Shule ya Msingi Mseto.

WAANDISHI WAPIGWA

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya waandishi wa habari walijikuta wakiwa katika wakati mgumu wa kufanya kazi zao baada ya kukamatwa na kupigwa na polisi.

Miongoni mwa waliopigwa ni Mwandishi wa Habari wa Chanel Ten, Vales Robert na Joel Maduka wa Stom Radio.

Akizungumzia tukio hilo, Robert alisema yeye na mwenzake walipigwa baada ya kushutumiwa na polisi, kwamba walikuwa wakipiga picha za tukio la Lowassa kukamatwa.

“Tulivamiwa na polisi wakati tukipiga picha na wakati tunapigwa, tulikuwa tumevaa vitambulisho vyetu vya uandishi wa habari.

“Yaani wamenivunjia kamera yangu, lakini nashukuru sijaumia sana,” alisema Robert.

KAMANDA WA POLISI

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Geita, Mwabulambo, alipopigiwa simu kuhusu suala hilo, simu yake ilipokewa na msaidizi wake ambaye alisema alikuwa katika kikao na Lowassa.

“Mimi ni mlinzi wa afande RPC, samahani yupo kwenye kikao na mheshimiwa Lowassa, nakuomba umtafute baadaye,” alisema bila kutaja jina lake.

Kutokana na tukio hilo, viongozi mbalimbali wa Chadema Mkoa wa Geita, walikuwa katika ofisi za Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Geita ili kujua hatma ya tukio hilo.

Kukamatwa kwa Lowassa na wenzake hao ni mwendelezo wa viongozi wa Chadema kukamatwa baada ya Januari 14, mwaka huu, Jeshi la Polisi, Mkoa wa Geita kumkamata Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Geita, Upendo Peneza.

Mbunge huyo baada ya kukamatwa, aliunganishwa kwenye kesi ya uchochezi na Diwani wa Kata ya Kasamwa, Fabian Mahenge wakituhumiwa kufanya uchochezi huo Januari 6, mwaka huu katika mkutano wa hadhara.

Kabla ya kumkamata Peneza, polisi waliwakamata Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika na Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Kagera, Conchesta Rwamlaza, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Anna Rose.

Tazama Video hapa chini Jinsi Lowassa alivyokamatwa na Polisi Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post