RAIS MAGUFULI AHUTUBIA UMOJA WA AFRIKA..JENGO LA MAKAO MAKUU YA AU KUITWA MWALIMU JULIUS NYERERE

Jengo la amani na usalama lililopo makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia jana tarehe 29 Januari, 2017 limetangazwa rasmi kuwa litaitwa Mwalimu Julius Nyerere.


Jengo hilo limepewa jina hilo rasmi katika hafla ya chakula cha mchana iliyofanyika leo na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Marais mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Antonio Guterres, Mawaziri na Mabalozi mbalimbali wanaohudhuria Mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaoendelea Mjini hapa.


Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli aliwashukuru viongozi wote wa Umoja wa Afrika kwa kuamua jengo hilo liitwe jina la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni kutambua mchango wake katika kupigania amani na usalama na amebainisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.


“Na kwa hakika naweza kusema kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora kabisa ambaye amewahi kutokea katika Bara letu, katika maisha yake yote Mwalimu Nyerere alipambana ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Afrika, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa umoja huu, sisi Watanzania kwa hakika tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa” alisema Mhe. Rais Magufuli.


Mhe. Dkt. Magufuli aliongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika kupambana na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa Taifa la Tanzania aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika nchi za Afrika.


“Wito wangu kwenu, waheshimiwa viongozi ni kwamba, sambamba na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama tutajitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya viongozi wengine hodari wa Bara hili wakiwemo Hayati Kwame Nkhrumah, Ahmed Ben Bella, Sekou Toure, Gamal Abdel Nasser na bila kusahau shujaa wetu mwingine Hayati Nelson Mandela” alisisitiza Rais Magufuli.


Mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaendelea leo tarehe 30 Januari, 2017 hapa Addis Ababa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527