RAIS MAGUFULI AENDELEA KUWALIPUA WAPIGA DILI TANZANIA

Rais John Magufuli ameendelea kupigilia msumari kwa watanzania na viongozi wasiopenda kujishughulisha na kuwajibika na kutegemea zaidi fedha za bure za umma.

Amehakikishia kuwa hali zao zitaendelea kuwa mbaya, isipokuwa kwa wale watakaowajibika na kujishughulisha.

Amesema wale wote wanaolalamika kuwa hawana fedha mfukoni kwa hivi sasa, walizokuwa nazo hazikuwa zao, ndio maana wanalalamika.

Katika hotuba zake mwaka jana katika sehemu mbalimbali nchini, Rais alisema wanaolalamika hawana hela mfukoni ni ‘wapiga dili’.

Rais alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano, itahakikisha inamaliza hali mbaya iliyokuwa inalikumba taifa la watanzania, ambapo watu wachache ndio waliokuwa wakinufaika na fedha za umma huku wananchi wengi wakiendelea kuumia na umasikini.

Alisema hayo mkoani Shinyanga jana wakati akizungumza na wananchi kuhusu maendeleo ya mkoa huo na kumbukumbu ya maadhimisho ya Miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

“Nimejitoa sadaka kwa ajili ya nchi hii, mimi sikuwa na urais ila mmenipa nyie, sasa nawaahidi mimi na serikali yangu tutawatetea kwa nguvu zote dhidi ya mafisadi.

"Nasikia kuna watu wanalalamika kuwa eti fedha hamna, kwani zilikuwa zinauzwa sokoni?" alihoji. 

Alisema watu wote wanaolalamika kuwa fedha zimepotea mitaani, ni wale waliokuwa wamezoea kupata fedha za bure bila kuzitolea jasho.

Aliwahakikishia kuwa wataendelea hivyo hivyo kutaabika, huku wale waliokuwa wakijishughulisha wakineemeka. Alisema fedha zilizotumiwa na mafisadi kipindi cha nyuma ni nyingi mno, kwani kila serikali ikitenga na kutoa fedha za maendeleo, zimekuwa zikiishia mikononi mwa mafisadi.

“Watu walikuwa wanajipatia tu fedha bila kuzitolea jasho, unakuta mtu anaenda nje kila siku, wapo waliofikia kufanyia mikutano ya taasisi zao za ndani nje ya nchi, mfano pale Muhimbili (hospitali ya taifa) nilipoenda nilikuta akinamama wanajifungulia chini huku fedha zipo lakini zimetengwa kwa ajili ya starehe,” alifafanua.

Alisema wakati serikali yake inaingia madarakani ilikuta nchi ina hali mbaya hali iliyoilazimu asafishe kila kona ya idara, ndipo walipopatikana watumishi hewa zaidi ya 18,000, wanafunzi hewa 65,000, mikopo ya elimu ya juu hewa yenye thamani ya Sh bilioni 3.5.

Alisema hata fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), zinazotolewa kwa kaya maskini, zilitolewa kwa kaya hewa 55,000.

Rais alisema ni wakati sasa Watanzania na serikali kwa ujumla wakashirikiana kuijenga Tanzania mpya, itakayomkomboa kila mwananchi akiwemo masikini, kwani kutokana na utajiri ambao Tanzania inayo, imekuwa ikichekwa kwa kuendelea kuwa masikini.

Utumbuaji majipu
Alisema pamoja na kwamba wapo baadhi ya watu wanachukizwa na hatua ya utumbuaji majipu kwa watumishi wasiowajibika, serikali yake itaendelea kuwatumbua watumishi na viongozi wanaokwenda kinyume na maadili yao.

“Ni bora nichukiwe na watu wachache kuliko kupendwa na wengi huku mambo yakienda mrama. Wale wote wanaodai mtindo wangu wa kutumbua ni mbaya hawa ndio majipu. Kabla ya utumbuaji watanzania walikuwa wanaishi maisha ya ajabu, na kusisitiza kuwa alikuwa mtumishi wa serikali kwa kipindi cha miaka 10 anajua anachoongea,” alisisitiza.

Aliomba Watanzania wamuombee ili aweze kuendeleza jitihada zake za kupambana na mafisadi kwani serikali yake ya awamu ya tano imejipanga kuendelea kuongoza kwa ukali kwa faida ya watanzania wote wakiwemo wanyonge na masikini.

“Lengo langu ni kuhakikisha wale wote waliokuwa wakila na kuchekelea kipindi cha nyuma wakati wenzao wanataabika, sasa waishi kama mashetani na wale waliotaabika waishi kama wafalme,” alisema.

Hatua za maendeleo
Dk Magufuli alisema kutokana na kutambua adha wanayoipata watanzania kutokana na huduma mbovu, serikali yake imejitahidi kupambana na kuboresha maendeleo mengi ikiwemo sekta za elimu, miundombinu usafiri na afya.

Alitolea mfano namna serikali hiyo ilivyofanikiwa kukusanya mapato kwa kubana maeneo yote yenye ubadhirifu na kufanikiwa kuongeza mapato kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh trilioni moja, hali iliyosaidia serikali hiyo kununua ndege sita, mbili zikiwa tayari zimewasili.

Pia alisema serikali imefanikisha kusimamia elimu bure kwa kutenga kiasi cha Sh bilioni 18.77 kila mwezi, zinazokwenda moja kwa moja shuleni kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi kusokma bure katika shule za msingi na sekondari.

Alisema pia serikali yake kwa kipindi kifupi, imefanikiwa kuongeza bajeti ya afya na kufikia Sh trilioni 1.99 na kati ya fedha hizo bajeti ununuzi wa dawa imeongezeka kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 250.

Mikakati
Aidha, kiongozi huyo alisema serikali yake imejipanga kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi, ambapo pamoja na kununua meli mbili katika Ziwa Victoria na Tanganyika, pia imeanza mchakato wa kujenga reli ya kisasa ambayo imetengewa jumla ya Sh trilioni moja katika bajeti ya mwaka 2016/17.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali za kutosha ikiwemo bahari, mito, maziwa, madini kama vile dhahabu na wanyama, lakini bado imeendelea kuwa na umasikini.

Alisema kutokana na hali hiyo, serikali yake imejipanga kuijenga Tanzania mpya ikiwemo viwanda ili kuweza kutimiza lengo la kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati.

“Hapa Shinyanga kuna mwekezaji ambaye ana takribani miaka 10 sasa tangu nikiwa waziri wa mifugo na uvuvi na baadaye ujenzi, hajaendeleza kiwanda cha nyama, naagiza uongozi wa mkoa wawekezaji kama hawa waondolewe wapewe wengine tusonge mbele,” alisisitiza.

Pamoja na mwekezaji huyo, pia alipotembelea mgodi wa Maganzo alipatiwa taarifa za kuwepo kwa migogoro ya ardhi na kuwataka mawaziri wa ardhi na mazingira, kushughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo.

Maji
Akizungumzia kero ya maji iliyowasilishwa mbele yake na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele, Dk Magufuli alibainisha kuwa atamtuma Waziri wa Maji kufuatilia bei inayotozwa kwa wakazi hao, ili kuwaondolea mzigo wa kutozwa bei kubwa ya maji.

Hata hivyo, Rais huyo aliweka wazi kuwa endapo atabaini bei inayotozwa kwa wakazi hao, haiendani na bei zinazotozwa katika miji mingine, atahakikisha ama anaipunguza au kuiongeza ili iendane na miji mingine.

Mapinduzi
Pamoja na hayo, Dk Magufuli alizungumzia maadhimisho ya siku ya mapinduzi ya Zanzibar na kubainisha kuwa kuanzia sasa serikali itakuwa inaadhimisha sikukuu za kitaifa katika mikoa mbalimbali ili kila mtanzania afaidike na sherehe hizo.

Alisema yeye na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein walipanga kila mmoja aadhimishe sherehe hizo katika maeneo tofauti, ambapo Dk Shein alikuwa visiwani Zanzibar yeye akiwa Shinyanga.

“Watu wamezoea wakisikia sherehe za kitaifa basi viongozi ni kulundikana sehemu moja. Sasa hili hatutolifanya, hizi ni sherehe za kitaifa kila mtanzania ana haki ya kuziadhimisha akiwa na viongozi wa kitaifa” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post