MGEJA AIONYA CCM KAGERA KWA ‘GOLI LA MKONO’


KADA machachari wa chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema) Khamis Mgeja amekionya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiache mchezo mchafu wa ‘Goli la Mkono’ ambao ni sawa na wizi wa kura katika chaguzi ndogo za Udiwani na Ubunge zinazofanyika nchini sasa.

Mgeja aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika kijiji cha Kiota kata ya Kimwani wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera wakati akimnadi mgombea udiwani kwa tiketi ya Chadema Leonard Nchimwani.

Kada huyo alisema wanazo taarifa kuwa CCM baada ya kuona
wameshaelemewa na wananchi wameshawachoka maeneo mengi nchini na dalili ya kushindwa iko wazi hivi sasa wameamua kujipanga kwa ‘Goli la Mkono’ ambao tunaona ni wizi wa kura.

“Ila mkakati wao wanaona,wanadhani utawaokoa kupita kila nyumba kugawa chumvi, khanga, fulana, kofia na sh 5,000 lakini pia imebakiza rasilimali za kubebwa lakini hawabebeki …..tunaiomba TAKUKURU ifuatilie ‘Tuhuma’ hizi kama kweli zina ukweli ndani yake hasa siku ya usiku wa kuamkia kupiga kura”,alisema Mgeja.

Alisema lakini tumejiandaa udhalimu wa mchezo mchafu wa goli la mkono kwani kauli hii ambayo iliwahi kutolewa na aliyekuwa katibu wa itikadi na uenezi taifa Nape Nnauye mwaka wa uchaguzi uliopita wa 2015, na sasa kuelekea katika chaguzi ndogo ,katika chaguzi za serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Mgeja alitahadharisha wapiga kura wanaounga mkono mabadiliko kuwa macho na kutokubali kununuliwa kwa ‘kitu kidogo’ na hatimaye kuuza haki yao ya kupiga kura na hatimaye kuwagharimu kwa kipindi cha miaka
mitano ijayo.

"CCM sasa hivi haina Pumzi imebaki kuweweseka na ile CCM ya Hayati Mwalimu Julias Kambarage Nyerere sasa hivi haipo..CCM ninayoifahamu mimi siyo hii iliyopo sasa imebaki jina tu la Bendera,leo watanzania mmeona tulipofika,pia mnaona mwenyekiti wa CCM taifa Dk John Pombe Magufuli anavyotumbua majipu kila wizara sasa lazima
tujiulize je! haya majipu nani kayafuga na kuyalea?…..wananchi
walipiga kelele kwa kujibu CC eeeeeeeeeeee M”,alisema.

Alisema hapa tulipofikia nchi kupinda ni chama cha mapinduzi (CCM) lazima ibebe lawama kwani wao ndio waliokabidhiwa kuongoza nchi wala siyo mtu.

Alisema ukiona wizi unatamalaki nchini,ufisadi,mishahara
hewa,makontena hewa,wanafunzi hewa na maeneo mengi ni uchafu ikiwemo mikataba mibovu ya madini, mwenyekiti wa CCM Dk John Magufuli alikuwemo na kwenye kikao muhimu cha baraza la mawaziri kwa kipindi cha miaka 20 yote haya hakuyaona.

Alisema hapa hawezi kukwepa lawama kwani naye alikuwemo kwenye hiyo nyumba ya CCM wakati uchafu huo unafanyika.

Mgeja alisema CCM wangekuwa waungwana ingewaomba radhi wananchi hapa ilipowafikisha ukiwemo umasikini mkubwa wa kutisha na rushwa iliyotamalaki na huko ndiko kuishiwa Punzi.

“Namuomba Katibu mkuu wa CCM taifa Abdulrahaman Kinana kwa niaba ya chama chake ajitokeze hadharani kwa niaba ya chama chake awaombe radhi wananchi kwa hapa CCM ilipotufikisha.

Kada huyo alisema watanzania wana kiu na hari ya mabadiliko kwa safari ya mabadiliko tayari tumeshafika na duniani sasa hivi wananchi wanataka mabadiliko kama vile nchi za Marekani,Gambia,Ghana na kwingineko wamefanya mabadiliko na mabadiliko kwa Tanzania ya sasa inawezekana.

Aidha Mgeja aliwaomba watanzania wajitambue,watambue haki zao za huduma za jamii kuwa ni wajibu wa serikali wala huduma hizo za jamii siyo hisani kutoka serikalini.

Mgeja aliwaomba wananchi wa kata ya Kimwani wamchague mgombea wa udiwani kupitia Chadema ili salamu ziwafikie CCM kuwa watanzania wamewachoka na wanataka mabadiliko.

Katika kampeni hizo ilihudhuriwa na mjumbe wa kamati kuu ya Chadema taifa Edward Lowassa,mbunge wa Chadema Wilfred Lwakatare,mstahiki Meya wa Bukoba Chifu Kalumuna,mkurugenzi wa fedha taifa wa Chadema Lodrick Lutembeka na viongozi wengineo wa chama hicho.

Na Hastin Liumba-Muleba

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post