ULIIPATA HABARI YA BWANA HARUSI KUMKIMBIA BI HARUSI KANISANI KABLA YA KUFUNGA NDOA?? MAPYA YAMEIBUKA

Mapya  yameibuka sakata la kukwama kufungwa kwa ndoa ya Samwel Mwakalobo na Ginen Mgaya, baada ya kubainika kuwa moja ya sababu ni Bibi harusi mtarajiwa kuendeleza uhusiano na mzazi mwenzake.

Bwana harusi, Samuel Mwakalobo alitoweka muda mfupi kabla ya kufunga ndoa na Ginen Mgaya  katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Isanga jijini Mbeya.

Mwakalobo (26) alizua taharuki hiyo  Ijumaa ya Desemba 16, baada ya kutoonekana kanisani kufunga ndoa mbele ya Mchungaji Andagile Mwakijungu.

Habari zimedai kuwa kabla ya mpango wa kufunga ndoa hiyo, Mgaya tayari alishapata mtoto kabla hajaolewa, na Bwana harusi kubaini dakika za mwisho kuwa wawili hao walikuwa bado wana uhusiano wa karibu.

Habari hizo za ndani kutoka familia ya Bibi harusi, zilidai kuwa kilichofanya Bwana harusi amtelekeze Bibi harusi ni wasiwasi aliokuwa nao juu ya uhakika wa ujauzito wa mkewe huyo mtarajiwa, kuwa ni wake kweli au wa mpenzi wake huyo wa zamani.

“Hofu hiyo ilijengeka kutokana na taarifa alizoziamini Bwana harusi kuwa Bibi harusi anaendeleza uhusiano na mzazi mwenziwe. Ni hofu tu ambayo angeifanyia kazi na angegundua kuwa haina ukweli wowote,”kilidai chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliendelea kudai: “Unajua muda mwingine binadamu tunahitaji kufanya uamuzi kwa kutafakari … maana shemeji yetu (Bwana harusi) alipigiwa simu na mzazi mwenza wa Bibi harusi na kuelezwa maneno ya ‘shombo’ na yeye bila kufanyia utafiti, akaamua kususa harusi.”

Wakati taarifa hizo zikibainisha hayo, familia ya Bwana harusi imeendelea kufanya jitihada za kuhakikisha suala hilo linamalizika kistaarabu.

Anayeelezwa kufuatilia suala hilo kwa karibuni ni kaka yake, ambaye hadi jana jitihada za kumtafuta mdogo wake zilikuwa zimeshindikana kutokana na kutopokea simu yake ya mkononi mara zote.

“Anayeongoza familia ya Bwana harusi ni kaka yake. Inasemekana pia kuwa wawili hao waliingia kwenye mgogoro dakika za mwisho kabla ya harusi na ndiyo maana baada ya kutoweka hataki hata kupokea simu,”kilieleza chanzo kingine.

Awali, mpambe wa Bibi harusi alieleza kuwa siku mbili kabla ya harusi hiyo, Bwana harusi alikuwa kwenye migogoro ya kifamilia na ndugu zake kuhusu fedha za sherehe na mpaka siku ya sherehe, suala hilo walikuwa hawajalitatua.

“Lakini tunashukuru kaka yake ni mstaarabu, aliamua kuonesha upendo kwa mdogo wake na amekuwa akilifuatilia suala hilo ili limalizike kwa amani, lakini mdogo mtu hapatikani,” alisema mpambe huyo.

Alisema jitihada za Bibi harusi kumtafuta Bwana harusi hazijazaa matunda, kwani hadi juzi alikuwa hapatikani hata nyumbani kwake, ingawa redio ilikuwa inasikika ndani ya chumba hicho kilichofungwa kufuli kwa nje.

Simu ya Bwana harusi ilikuwa ikiita muda mwingi bila kupokewa, lakini hatua zingine zilidai kuwa Bwana huyo ambaye ni mfanyabiashara kwenye kituo cha mabasi yaendayo Chunya eneo la Isanga jijini Mbeya hajafungua duka lake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post