Serikali yatengua umiliki wa Shamba la Mifugo la Manyara,Waziri Mkuu Alikabidhi kwa Wananchi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemkabidhi hati ya shamba la mifugo la Manyara, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Stephen Ulaya baada ya kubadilisha umiliki wa shamba hilo.

Umiliki ulibadilishwa kutoka Taasisi ya Tanzania Land Conservation Trust (TLCT) ambayo mwenyekiti wa bodi yake ni Mbunge wa zamani wa Monduli, Edward Lowassa kwenda kwa wananchi wa vijiji viwili vya Elesilalei na Ortukai vya kata ya Elesilalei, eneo la Makuyuni, wilayani hapa.

Hatua ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi ni baada ya kilio cha muda mrefu kwa wananchi hao kudai kuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliagiza shamba hilo ligawiwe kwa wananchi lakini haikuwa hivyo, badala yake watu wachache walijimilikisha kinyemela chini ya wenyekiti wa bodi ya TLCT.

Majaliwa alitangaza kukabidhiwa hati hiyo wakati alipomtembelea mwanzilishi wa Shule ya Msingi Laibon, Leshuko ole Mapii, kata ya Elesilalei.

Alifika kujionea hali halisi ya mwamko wa elimu kwa mzee huyo ambaye wajukuu zake na watoto wake zaidi ya 102 wanasoma shuleni hapo pamoja na watoto wengine wanaotoka jirani na eneo hilo.

Alisema serikali imeamua kurudisha shamba hilo kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili baada ya Baraza la Madiwani na uongozi wa wilaya hiyo ya Monduli kuridhia kwa pamoja umiliki wa shamba hilo kurudi kwa wananchi.

Alisema shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 44,930 lilikuwa likimilikiwa na TLCT linalofadhiliwa na Shirika la African Wildlife (AWF), hivi sasa ni mali ya wananchi na halmashauri ya Monduli ndio wataamua kupanga matumizi bora ya ardhi.

Alisema nyaraka zinazoonesha kuwa shamba hilo lililotolewa kwa wananchi wa vijiji vya Elesilalei na Ortukai na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu mwaka 1999 kwa ajili ya kilimo na ufugaji lakini hakuna kilimo chochote hapo na badala yake TLCT ikajimilikisha shamba hilo kinyume na maagizo.

"Sasa namkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli hati hii na kuanzia leo(jana) umiliki wa shamba hilo utakuwa chini ya halmashauri na wananchi mtaamua kupanga matumizi bora ya ardhi katika shamba hili mliloteseka nalo kwa muda mrefu," alisema.

Alisema serikali itawanyang'anya mashamba wale wote wanaomiliki bila ya kuyaendeleza kwa kuwapa wananchi na kuhoji ni kwa nini wenye fedha kuchukua mashamba mkubwa bila ya kuyaendeleza.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kabla ya ujio wa Waziri Mkuu, alifanya ziara katika shamba hilo na kuagiza uongozi wa wilaya ya Monduli, mkoani Arusha na baraza la madiwani la wilaya hiyo kuhakikisha wanabadilisha umiliki wa shamba hilo kwenda kwa wananchi wa vijiji husika kama Rais mstaafu, Benjamini Mkapa, alivyoagiza.

Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema) pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Isack Joseph kwa nyakati tofauti waliishukuru serikali kwa uamuzi huo na kuipongeza serikali kwa kujali maslahi ya wananchi wake.

Mkurugenzi wa TLCT, Boniface Ngimojiro alipopewa nafasi ya kusema neno kwa wananchi hao, alisema taasisi hiyo inaongozwa na bodi ya wadhamini yenye wajumbe wanane wakiongozwa na Mbunge wa zamani wa Monduli, Edward Lowassa kama mwenyekiti wa bodi hiyo.

Aidha alikiri kupata amri ya kubadilishwa umiliki wa shamba hilo kutoka katika taasisi hiyo kwenda kwa wananchi wa vijiji hivyo viwili na kusisitiza kuwa kwa sasa ameridhia shamba hilo kumilikiwa na wananchi.

Meneja wa AWF, Fidelis Ole Kashe, alisema wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu ndani ya shamba hilo pamoja na kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye shamba hilo ikiwemo shule, zahanati, ufugaji wa kisasa na machinjio.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, aliwasihi wananchi hao kuheshimu njia za mapito ya wanyama katika eneo hilo ambalo wanyamapori kutoka hifadhi za Tarangire, Manyara na Ngorongoro wanalitumia kwa ajili ya kupita kwenye hifadhi hizo mara kwa mara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post