MBUNGE WA CHADEMA ANUSURIKA KUFA AJALINI...GARI LAKE LAUA MTOTO

Gari la Mbunge wa Mbeya mjini Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Sugu) Toyota Land Cruser T.161 CPP likiwa ofisi za Usalama barabarani jijini Mbeya baada ya kugonga mtembea kwa miguu na kusababisha kifo.
Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi (SUGU)

Na JamiiMojaBlog,Mbeya

Mkazi wa Iyunga jijini Mbeya ambaye amefahamika kwa jina moja la Rechal (13) amefariki dunia mara baada ya kugongwa na gari , namba T161 CPP Toyota LandCruiser inayodaiwa kumilikiwa na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi maharufu kwa jina la (SUGU), kwenye kivuko cha barabara (ZEBRA) na kumsababishia kifo chake papo hapo.

Tukio hilo limetokea leo Desemba 17 majira ya saa mbili asubuhi huko katika eneo la Iyunga Jijini hapa, wakati gari ya Mbunge huyo ikiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege wa Songwe kwa ajili ya mapokezi ya kiongozi wa Kitaifa Freeman Mbowe.


Imeelezwa kuwa, gari hilo likiwa katika mwendokasi linadaiwa kukiuka sheria za barabarani kwa kutosimama kwenye kivuko cha barabara kinachowaruhusu watembea kwa miguu kuvuka na kumgonga mtoto huyo na kusababisha kifo chake papo hapo.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema mtoto huyo akiwa na mama yake walikuwa wakivuka barabara baada ya magari ya upande wa pili kusimama na kuwaruhusu watembea kwa miguu hao kuvuka.


Wamesema, wakiwa katikati ya kivuko hicho mama wa marehemu alishangaa kuliona gari ya Mbunge hiyo ikija kwa kasi hivyo kumuachia mtoto wake aliyekuwa amemshika mkono na yeye kutafuta njia ya kujiokoa.


Wameeleza kuwa licha ya dereva wa gari ya Mbunge kuona madereva wenzie wa magari yaliyokuwa yakitokea Mbalizi wakisimama kwa ajili ya kuwaruhusu watembea hao kuvuka lakini yeye akitokea mjini Mbeya alishindwa kutii sheria hiyo na kupita akiwa katika mwendo kasi.

“Madereva wenzie tumesimama ili mama na mtoto wavuke lakini yeye akiwa na haraka alipita tu, kwa kweli hii inauma sana, nasikia mtoto amepoteza maisha lakini mama amejeruhiwa na kwamba amekimbizwa hospitali Teule ya Ifisi kwa matibabu,”alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari akizungumza kwa njia ya simu amekiri kutokea kwa tukio hilo na kuthibitisha kifo cha mtoto huyo.

Aidha Kivadashari ametaja jina la dereva wa gari hiyo kuwa ni Gabriel Endrew maarufu Dj BBG (43) mkazi wa Mwakibete jijini Mbeya.

Pia, aliongeza kuwa gari hiyo imekamatwa na dereva anashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post