MADEREVA WANAOPANDISHA NAULI MSIMU HUU WA SIKUKUU WADHIBITIWE


DESEMBA kila mwaka ni mwezi ambao familia nyingi zinaungana, kwa kuwa wafanyakazi wengi hupenda kuchukua likizo na wanafunzi hufunga shule kwa ajili ya likizo ndefu.
Kutokana na sababu hiyo, familia nyingi hupenda kusafiri kwenda maeneo tofauti kwa ajili ya kubadilisha mazingira. Zamani wenyeji wa mkoa wa Kilimanjaro, walikuwa na utamaduni kuwa ifikapo mwezi huu ni lazima waende kwao kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Lakini, katika miaka ya hivi karibuni, hali hii imesambaa katika mikoa yote ya Tanzania, ambapo familia huenda kusherehekea sikukuu hizo na wazazi ama ndugu zao vijijini.
Kutokana na utamaduni huu, uliojengeka kwa familia nyingi nchini kwa mwezi huu wa Desemba, wamiliki wa mabasi yaendayo mikoani, wamekuwa wakiona hilo ndilo eneo lao pekee la kuchuma kwa haraka kwa kupandisha sana nauli za mabasi.
Nauli hizo hupanda kila mwaka kuanzia tarehe 15 mwezi huu, kutokana na watu kusafiri kwa wingi. Kipindi hicho wamiliki hao wa mabasi hupandisha nauli kila siku kulingana na idadi ya watu inavyozidi kuongezeka. Wenye mabasi huita msimu huo kuwa wa neema ama wa mavuno kwa sababu hutoza nauli kubwa, kwa kuwa wanaelewa ni lazima watapata abiria.
Nauli hizo kwa kweli zimekuwa ni maumivu makubwa kwa abiria wengi, hasa wale wenye kipato cha chini. Kwa mfano miaka iliyopita, nauli ya kwenda Kilimanjaro au Arusha ilikuwa ni kati ya Sh 20,000 na Sh 30,000, lakini inapofikia kipindi hiki cha ‘mavuno’, hupanda hadi kufikia Sh 50,000 hadi 70,000.
Kwa wale wanaosafiri mwezi huu wa Desemba, watakubaliana nami kuhusu nauli hizo, kwani kama nilivyoeleza hapo juu kwa sasa umekuwa ni utamaduni kwa watu wa mikoa yote kwenda kusherehekea sikukuu kule walikozaliwa.
Mfano mzuri upo katika stendi kuu ya mabasi ya mikoani ya Ubungo jijini Dar es Salaam, ambapo katika kipindi cha kuanzia Desemba 15 mpaka 24, mara nyingi mabasi huwa yameshajaa, yaani abiria wanakuwa wameshakata tiketi mapema.
Lakini pia kumekuwa na mchezo mchafu kwa baadhi ya watu wanaojiita mawakala wa mabasi. Wao wamekuwa wakinunua tiketi hizo mapema kwa lengo la kuziuza kwa bei ya juu. Na kipindi hiki abiria huwa wengi katika kituo hicho cha mabasi kwa kuwa wanakosa usafiri wa kwenda kule wanakoelekea.
Jambo hili tumekuwa tukilishuhudia kwa miaka yote, japokuwa miaka mitatu hivi iliyopita Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imelivalia njuga kwa kuwatoza faini wote wanaoongeza bei, hatua ambayo imepunguza kidogo adha hiyo.
Nasema Sumatra imepunguza kidogo adha hiyo kwa sababu wanapokagua vitabu vya nauli vya mabasi hayo, huwa vinaonesha vimeuzwa kwa bei ile ya kawaida, lakini wananchi wengi wanalalamika kuuziwa na mawakala nauli hizo kwa bei ya juu. Ombi langu kwa Sumatra ni kuhakikisha inadhibiti hali hii isitokee mwaka huu.
Itumie mbinu zote kuwakamata wajanja wachache wanaoumiza wananchi kwa kuwalangua tiketi katika msimu huu wa sikukuu, ambao wao wanauita msimu wa mavuno.
Ili kukomesha hali hii ni vema abiria watoe taarifa mapema pale wanapokutana na adha hiyo, japo wengine wanaona ni sawa kwa kuwa wanakuwa wameshajiandaa kusafiri na wana uwezo wa kulipa nauli yoyote. Nina hakika kama wananchi watashirikiana vizuri na vyombo vya dola, hakutakuwa na ongezeko holela la nauli katika msimu huu wa Krismasi na Mwaka Mpya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post