Maajabu Duniani!! KUTANA NA MAKABURI YA KIFAHARI YANAYOZIDI NYUMBA ZA MATAJIRI...YANA HADI VIYOYOZI

Maishani, watu wengi hutaka kuishi katika nyumba nzuri na za kifahari. Wengi huwa hawafanikiwi. Lakini nchini Mexico, ambapo ulanguzi wa mihadarati umekithiri, wakuu wa magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya huishi maisha ya kifahari, na huendeleza hizi hata wanapokuwa wafu.

Nchini humo, utapata makaburi ambayo yangegeuzwa kuwa nyumba, matajiri wengi wangejivunia kuishi.

Ni makaburi makubwa yaliyojengwa na kuwekwa huduma za kisasa na vitu vingi vya anasa.

Kuna baadhi ya makaburi yenye viyoyozi vya kudhibiti viwango vya joto na kuingiza hewa safi, kuna vioo visivyopenya risasi na baadhi yana hata vyumba ambavyo wageni wanaofika kutoa heshima kwa wafu, wanaweza kuketi na kupata kila kitu kinachopatikana katika nyumba za kifahari.

Baadhi yanakadiriwa kugharimu hadi £230,000 (Sh633 milioni za Tanzania; Sh29 milioni za Kenya)

Hali hii ni tofauti kabisa kwa maelfu ya watu wanaouawa katika makabiliano ya magenge ya ulanguzi wa dawa hizo za kulevya ambao sana huzikwa katika makaburi ya pamoja au miili yao kutungikwa na kuachwa ikiwa imening'inia kwenye madaraja.
Ni mwongo mmoja sasa tangu serikali ya Mexico ilipotuma wanajeshi wake kwenda kukabiliana na magenge ya walanguzi.

Lakini walanguzi wakuu, ambao wamejipatia pesa nyingi, wanaweza kupamba makaburi yao kutokana na pesa walizolimbikiza kutokana na biashara hiyo.

Makaburi mengi haya hupatikana jimbo la Sinaloa, anamotoka mlanguzi mkuu Joaquin "El Chapo" Guzman ambaye kwa sasa anazuiliwa na anatarajiwa kuhamishiwa Marekani mwakani.

Katika eneo moja la makaburi, Jardines del Humaya, katika mji mkuu wa jimbo la Culiacan, ndipo unapopata baadhi ya makaburi ya kupendeza zaidi.
"Ni ishara ya nguvu na mamlaka ambayo wakati mmoja walikuwa nayo na ni ishara ya matamanio yao ya kutaka kuishi daima, jambo ambalo ni kawaida kwa binadamu yeyote yule," anasema Juan Carlos Ayala, profesa wa falsafa katika chuo kikuu cha Autonomous University cha Sinaloa ambacho huangazia sana utamaduni wa ulanguzi wa dawa.

"Pia ni onesho kwa wale ambao wanaendelea kuishi kwamba mtu huyu alikuwa mtu mashuhuri."
Mwendelezo wa filamu za Netflix, Narcos, umekuwa ukitoa kidokezo kwa wengi duniani kuhusu maisha yalivyo kwa walanguzi wa mihadarati.
Lakini nchini Mexico, serikali inatafakari uwezekano wa kupiga marufuku filamu kama hizo, kama njia ya kuwazuia watoto kutazama maisha ya ulanguzi wa mihadarati kama ya kuvutia.

"Ulanguzi wa mihadarati unakolea katika jamii, kupitia utamaduni, na sasa tuna tatizo la kutazama umeanzisha wapi na umefikia mwisho wapi," alisema Ayala.

Kaburi moja ambalo linadaiwa kuwa na mwili wa mlanguzi aliyetumiwa kuua watu, lina hata kamera za kiusalama, pamoja na kioo kisichopenya risasi.

Lina pia kuba lenye taa ambazo huwaka. Ndani kuna visu vinne vilivyofungiwa kwenye kijisanduku kilichoundwa kwa vioo.

Baadhi ya makaburi yamejengwa kama nyumba za kisasa au makanisa madogo. Krismasi inakaribia, na baadhi hata yamewekewa miti bandia ya Krismasi.

Lakini kinachokosekana katika makaburi mengi ni utambulisho wa aliyezikwa ndani.
Santa Muerta, mtakatifu wa kifo, ambaye hatambuliwi na Kanisa Katoliki la Kirumi, hutukuzwa sana na mamilioni ya watu Mexico, wakiwemo wahalifu.

"Kuna mchango mkubwa wa dini katika utamaduni wa ulanguzi wa dawa, kwa sababu iwapo kuna mtu anayehitaji sana ulinzi kutoka kwa miungu au Mungu, basi ni mlanguzi wa mihadarati ambaye anaweza kuuawa kwa kupigwa risasi na magenge hasimu au maafisa wa serikali wakati wowote," anasema Andrew Chesnut, mwandishi wa kitabu kwa jina Devoted to Death: Santa Muerte, the Skeleton Saint (Kujitolea kwa Kifo: Santa Muerte, Mtakatifu wa Kiunzi cha Mifupa).

Chanzo-BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post