JAMBAZI SUGU AUAWA AKIJARIBU KUTOROKA POLISI SHINYANGA

Mwanamme mmoja anayedaiwa kuwa ni jambazi sugu  aliyejulikana  kwa jina la Amos James Haruna mkazi wa mtaa wa Nyahanga  wilayani Kahama mkoani Shinyanga ameuawa   kwa kupigwa risasi na  askari wa jeshi la polisi , wakati akijaribu kutoroka  huku wengine nane wakishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa kutumia silaha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini  kwake leo  Desemba 3,2016,  kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amesema  kulingana na kumbukumbu za wahalifu za polisi ndipo walibaini mtu huyo alikuwa ni jambazi sugu kutokana na kufanya uhalifu katika mikoa ya kanda ya ziwa.

Amesema jambazi huyo  alikutwa na silaha aina ya SMG yenye namba K5380 ikiwa na risasi 30 na zingine nane zikiwa kwenye mfuko akiwa kwenye gari yake yenye namba za usajili  T 794 BZP Toyota Cresta  alipohojiwa  alikiri kufanya uhalifu mikoa ya Mwanza,Geita na Shinyanga.

“Polisi baada ya kumuhoji  jambazi huyo sugu Novemba 30 mwaka huu aliwaeleza kuwa anayo bunduki nyingine aina ya SMG ambayo alidai huwa anaificha kwa mganga wa kienyeji e kijiji cha Busoka  halmashauri ya mji wa Kahama aliondoka na polisi na alipokaribia eneo hilo kwenye mkusanyiko wa  watu aliwaeleza wasimame na kushuka ndipo alipojaribu kutoroka na kupigwa risasi”anaeleza kamanda Muliro.

Kamanda Muliro alisema watuhumiwa wengine nane wamekamatwa wakiwemo wanawake wanne na wanaume wanne.


Na Stella Ibengwe-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post