Serikali amewaagiza wote waliohitimu kidato cha sita Mei mwaka huu na ambao hawajajiunga na vyuo vya elimu ya juu, wakaripoti katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Desemba Mosi, mwaka huu.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi ametoa agizo hilo mjini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Habari wa Bunge.
Dk Mwinyi alisema Mei na Juni mwaka huu, JKT iliwafanyia usaili vijana wa kujiunga na JKT kwa kujitolea. Alisema usaili huo ulifanyika kwa kushirikiana na kamati za ulinzi za wilaya na mikoa.
“Wizara ya Ulinzi na JKT inapenda kuwatangazia vijana wote waliosailiwa Juni mwaka huu, kujiunga na JKT kwa kujitolea, waripoti kwenye kambi walizopangiwa ifikapo Desemba Mosi mwaka huu kwa nauli zao,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amesema mafunzo hayo ni ya miezi mitatu kwa mafunzo yenye utaratibu wa kawaida na miaka miwili kwa wa kujitolea.
Ili kufanikisha hilo, Wizara ilimuagiza Mkuu wa JKT kufufua kambi ya Makuyuni JKT iwe miongoni mwa kambi kuanzia Desemba mwaka huu.
Aliagiza kambi za Luwa na Milundikwa za mkoani Rukwa, zirejeshwe kwa shughuli za JKT za kilimo na ufugaji.
Dk Mwinyi alimuagiza Mkuu huyo wa JKT pia kambi ya Mpwapwa irejeshwe kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya kilimo na ufugaji ndani ya JKT.