MKE WA RAIS MAGUFULI ATOKA HOSPITALI YA MUHIMBILI ALIKOKUWA AMELAZWA

Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Sewahaji ya Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam ameruhusiwa na kurejea nyumbani leo tarehe 11 Novemba, 2016 baada ya afya yake kuimarika.

Kabla ya kuondoka katika wodi ya Sewahaji alikokuwa amelazwa Mama Janeth Magufuli amewashukuru Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu mazuri aliyoyapata na pia amewashukuru Watanzania wote kwa kumuombea afya njema.

"Namshukuru sana Mungu kwamba afya yangu imeimarika, pia napenda kuwashukuru Madaktari na Wauguzi, nimepata huduma nzuri sana maana siku nilipoletwa hapa nilikuwa sina fahamu na hali yangu ilikuwa mbaya lakini mmenipigania na leo narudi nyumbani nikiwa na afya imara.

"Naomba pia niwashukuru Watanzania wote kwa kuniombea, nawahakikishie kuwa sasa nipo vizuri na madaktari wameniruhusu nirudi nyumbani ambako nitamalizia matibabu yangu" amesema Mama Janeth Magufuli.

Mama Janeth Magufuli alilazwa hospitalini hapo tangu Juzi tarehe 09 Novemba, 2016 baada ya kuugua ghafla na kupoteza fahamu.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
11 Novemba, 2016


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post