MCHUNGAJI LUSEKELO 'MZEE WA UPAKO' AKAMATWA NA POLISI KWA KUMFANYIA FUJO JIRANI YAKE..YADAIWA ALIKUWA AMELEWA

Mchungaji  Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Dar es Salaam, Anthony Lusekelo, maarufu Mzee wa Upako, amekamatwa na polisi akituhumiwa kumfanyia fujo na kutishia kumuua jirani yake.

Tukio hilo lilitokea juzi maeneo ya Kawe wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa tatu alipochukuliwa na polisi wa Kituo cha Kawe.

Wakati wa tukio hilo, Mchungaji Lusekelo alikuwa ameegesha gari lake barabarani kiasi cha kusababisha usumbufu na foleni ya magari mengine.

Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa ni kulipiza kisasi kwa jirani zake hao wanaoishi katika nyumba namba KAW/MZN/1348, ambao alidai wamekuwa wakimkebehi kuwa hafai kuwa mchungaji kwa sababu ya ulevi.

Licha ya baadhi ya watu kumsihi aondoke eneo hilo kutokana na hadhi yake, mchungaji huyo alikaidi, huku akiendelea kuongea kwa sauti iliyofanana na mtu mwenye kilevi.

Baadhi ya maneno yaliyosikika kwenye video iliyorekodiwa eneo la tukio  hayaandikiki  kwa kuwa si ya kawaida.

“Mjinga wewe, mimi ni zaidi ya askari na wewe ni mgambo, na si mgambo wewe ni raia tu.

“Umenitukana sana wewe mpaka leo nimeamua kuloana na mvua, usitoe gari hapo mshenzi sana wewe, na nikikuona mahali popote…, mshenzi kabisa, muangalie sana huyo,” alisikika Mchungaji Lusekelo akiongea kwa sauti.

Baada ya kuongea maneno hayo, ilisikika sauti ya mwanamke kutoka ndani ya uzio wa nyumba hiyo ikimjibu mchungaji huyo: “Huwezi, aniangalie kitu gani.”

Hata hivyo, hata watu mbalimbali walipomsihi aache kutoa lugha hizo za kejeli na aondoe gari lake lililokuwa limesababisha foleni, alikataa akisema hataliondoa hadi atakapokuja Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro.

Baada ya purukushani hizo, polisi kutoka katika Kituo cha Kawe walifika eneo hilo saa tatu asubuhi, wakamchukua mchungaji huyo na kumpeleka kituoni.

Inadaiwa baada ya kufikishwa kituoni hapo, mchungaji huyo alipimwa kiwango cha ulevi na kukutwa 131, ambacho kinaelezwa kuwa ni kikubwa – ulevi wa kupindukia.

Ilipofika saa tano asubuhi, mchungaji huyo alihamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), ambako huko nako inadaiwa alipimwa kilevi na kuonekana kushuka hadi kufikia 121.

Alipotafutwa Kamishna Sirro ili kuzungumzia sakata la mchungaji huyo, alisema atalizungumzia leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527