KUHUSU KIFO CHA ALIYEWAHI KUWA WAZIRI WA ELIMU TANZANIA ,JOSEPH MUNGAI

Mwanasiasa mkongwe na waziri wa zamani wa Serikali ya awamu ya kwanza hadi ya nne, Joseph Mungai, amefariki dunia.

Mungai aliyezaliwa Oktoba 24,1943 alifariki dunia   Dar es Saalam  jana baada ya kuugua kwa muda mfupi.
 
Akisimulia mazingira ya kifo cha baba yake, mtoto wa marehemu, William Mungai, jana alisema baba yake alifariki dunia wakati akipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.

Alisema kabla ya kifo hicho baba yake alianza kulalamika kuumwa na tumbo na kutapika ambako alipelekwa katika hospitali moja ambayo hakutaka kuitaja.

Alisema baada ya kufikishwa hospitalini hapo, hali yake ilizidi kubadilika na kuwa mbaya zaidi na hivyo wakaamua kumkimbiza Muhimbili kwa matibabu zaidi.

“Ni kweli baba amefariki dunia saa 10 jioni leo (jana) wakati tukimpeleka Muhimbili baada ya kulalamika kuumwa na tumbo. Hivi tunavyoongea, ndiyo tunatoka Muhimbili ila taarifa zaidi tutawapatia baada ya kikao cha ndugu,” alisema William kwa kifupi.

Ingawa William hakutaka kuzungumzia kifo hicho kwa undani, taarifa zilizopatikana na ambazo hazijathibitishwa, zinasema kiongozi huyo alikunywa kinywaji katika hoteli moja maarufu ya  Dar es Salaam.

Watu walio karibu na familia ya Mungai mameeleza  kuwa, jana mchana Mungai alikuwa katika hoteli hiyo iliyopo Msasani akipata kinywaji kwa kuwa alikuwa na mazoea ya kufika mahali hapo.

“Mzee jana alikuwa katika hoteli hiyo akiendelea na kinywaji akipendacho cha whisky. Inasemekana baada ya kutoka hotelini hapo na kurudi nyumbani kwake, alianza kutapika huku akilalamika kusikia maumivu makali ya tumbo.

“Vijana wake walimpeleka hospitali ya karibu, lakini hali ilizidi kuwa mbaya ndipo familia iliamua kumkimbiza Muhimbili ambako aliaga dunia,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Mungai  aliwahi kuwa Mbunge wa Mufindi kupitia CCM kwa miaka 35.

Pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini enzi za utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na pia katika awamu za pili, tatu na nne.

Baadhi ya nyadhifa alizowahi kushika kwa nyakati tofauti ni uwaziri wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post