KUHUSU KIBANO WAHITIMU ELIMU YA JUU,WAAJIRIWA KUONJA MACHUNGU


SHERIA mpya ya kulipa mikopo kwa wahitimu wa elimu ya juu iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni, itazidisha machungu kwa waajiriwa wapya na wale wa zamani.


Kwa mujibu wa sheria hiyo, wakopaji hao wataanza kukatwa deni hilo moja kwa moja kutoka kwenye mishahara yao baada ya miaka miwili tangu walipomaliza masomo yao.


Kwa mujibu wa sheria hiyo, wakopaji ambao tayari wamehitimu na kuajiriwa watakutana na kibano katika kulipa deni hilo kwa kukatwa asilimia 15 ya mshahara wao.


Mbali ya makato hayo, mtumishi mpya ambaye ataajiriwa baada ya kumaliza masomo yake, mshahara wake pia itabidi ukatwe kodi ya mapato (Payee) pamoja na makato mengine yakiwamo ya mifuko ya jamii, chama cha wafanyakazi na bima ya afya.


Mathalani, muhitimu wa Shahada ya kwanza ya udaktari ambaye kwa mujibu wa sheria anapokea mshahara wa Sh 1,480,000, baada ya makato atabakiwa na wastani wa Sh 754,300.


Katika mchanganuo huo, mwajiriwa atakatwa asilimia 15 kodi ya mapato, sawa na Sh 326,000, Sh 148,000 ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), deni la mkopo wa HESLB Sh 222,000.


Katika orodha hiyo, pia kuna makato ya Sh 29,600 ya chama cha wafanyakazi mbali na makato ya Bima ya Afya ambayo mfanyakazi hukatwa kulingana na mshahara wake.


Watumishi wengine watakaokumbana na panga hilo la makato ni walimu na wauguzi ambao wamenufaika au watanufaika na mkopo huo wa Serikali.


Kwa mwalimu mwenye Shahada ambaye mshahara wake unaanzia Sh 716,000 atalazimika kubaki na Sh 565,500 huku mwenye Stashahada ambaye mshahara wake wa kuanzia ni Sh 530,000 atabakiwa na wastani wa Sh 440,000 baada ya makato yote, kwa mujibu wa sheria.


Wakati huohuo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jana ilitangaza kuwasaka kwa udi na uvumba wadaiwa wote sugu 142,470 ili wafikishwe mahakamani.


Wadaiwa hao ni walionufaika na mkopo tangu mwaka 1994-1995 hadi Juni mwaka huu na kufikisha deni la zaidi ya Sh 239,353,750,176. 27.


Ili kuhakikisha fedha hizo za mikopo zinapatikana, HESLB itawasilisha majina ya wadaiwa hao kwenye taasisi za fedha ili kutathmni tabia zao kabla ya kukopeshwa au kuwadhamini.


Akizungumza Dar es Saalam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru alisema kuanzia sasa wadaiwa hao na wadhamini wao wanapaswa wajisalimishe kwa bodi hiyo vinginevyo watafikishwa mahakamani.


“HESLB inatoa notisi ya siku 30 kwa wadaiwa hao walipe kiasi chote cha madeni yao baada hapo watafikishwa mahakamani.


Hata hivyo, alisema Sh 51,103,685,914 ni deni lililorithiwa kutoka kwa iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambazo zilizokopeshwa kwa wanafunzi 48,378 tangu mwaka 1994 hadi Juni mwaka 2005.
Badru alisema kuanzia Julai, mwaka 2005 hadi Juni 30, mwaka huu Bodi imetoa Sh 2,544,829,218,662.50 kwa wanafunzi 330,801.


Hali hiyo inafanya jumla ya fedha zilizokopeshwa tangu mwaka 1994/95 hadi 2015/2016 kufikia Sh 2,595,932,575.56 ambako wanafunzi 379, 179 wamenufaika nazo.
Badru alisema kati ya mikopo yote iliyotolewa kuanzia mwaka 1994/95 mpaka Juni mwaka huu, mikopo iliyoiva ni Sh 1,425,782,250,734.31 ambayo ilitolewa kwa wanufaika 238,430.


Mkurugenzi Msaadizi wa Mikopo kutoka HESLB, Dk. Abdul Mussa Ally alisema hali ya urejeshaji wa mikopo ni nzuri.


Alisema katika mwaka wa fedha uliopita, Sh bilioni 36 zimekusanywa na Julai hadi Oktoba mwaka huu zimekusanya Sh bilioni 25,000.
Ally alisema ukusanyaji wa fedha hizo umezidi kuongezeka kutoka Sh bilioni mbili kwa mwezi hadi Sh bilioni sita hadi saba kwa mwezi hivi sasa.


Imeandikwa na CHRISTINA GAULUHANGA Na MAULI MUYENJWA-MTANZANIA DAR ES SALAAM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post