Kimenuka!! KIGOGO WA CCM AANIKA MADUDU KATIKA MANISPAA YA SHINYANGA,AJIUZURU KAMATI YA FEDHA,MSIKILIZE HAPA AKIFUNGUKA



Aliyekuwa Naibu mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga na sasa diwani wa kata ya Ndembezi katika manispaa ya Shinyanga David Mathew Nkulila (CCM) ametangaza kujiuzuru ujumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala ili kufikisha ujumbe kwa umma kwamba hakubaliani vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma unaofanyika katika manispaa ya Shinyanga.

Miongoni mwa hoja zilizomfanya ajiuzuru ni sakata la Greda aina TEREX T180 mali ya Halmashauri Manispaa ya Shinyanga,hoja za barabara za lami mjini Shinyanga,hoja kuhusu JASCO,udanganyifu wa Bajeti 2016/17 ulioanzishwa na Baraza la madiwani na uliowasilishwa wizarani sambamba na ujenzi wa nyumba za ghorofa mjini kati na usimamizi wake.

Mwenyekiti wa kamati ya fedha na utawala katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga,ambaye pia mstahiki meya wa manispaa hiyo Gulam Hafeez Mukadam amesema  hapingani na taarifa za wataalam waliochunguza kuwa greda lililonunuliwa na manispaa hiyo kuwa ni zima/halina tatizo.

Hata hivyo amesema bado hajapata taarifa wala barua kuhusu kujiuzuru kwa mjumbe yeyote wa kamati anayoiongoza.

Msikilize hapa Mheshimiwa David Nkulila akizungumzia Utata wa Greda la Manispaa ya Shinyanga lililonunuliwa shilingi milioni 520

Hii hapa ni taarifa aliyoitoa leo Jumatatu,Novemba 28,2016 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu wanahabari, leo tarehe 28/11/2016 nimeona ni vema kuwaita mimi kama Diwani wa Kata ya Ndembezi, Mjumbe wa Baraza la Madiwani Manispaa ya Shinyanga na mtumishi wa umma kwa ujumla ili nizungumze nanyi /baada ya kujiuliza maswali mengi sana, na kuyatafakari juu ya utata wa mambo kadhaa yanayojitokeza manispaa na yenye athari kwa wakazi walionipa dhamana ya udiwani  kwa uaminifu. Tarehe 10/12/215, katika baraza la kwanza niliapishwa kwa maneno haya na ninanukuu.

“Mimi Nkulila David Mathew naapa kwa dhati kwamba; nitaitumikia Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kwa wadhifa wangu wa UDIWANI na kwamba NITAHIFADHI, NITALINDA na KUTETEA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA sheria za Tanzania, maadili ya madiwani na kanuni za kudumu za halmashauri, kama zilivyowekwa kwa mujibu wa sheria, na kwamba nitaitumikia Halmashauri ya manispaa ya Shinyanga kwa waminifu na moyo wangu wote (Ee Mwenyezi Mungu nisaidie)”

Pengine ni vema kueleza wazi kwamba nimeamua kujiuzuru ujumbe wa KAMATI YA FEDHA NA UTAWALA ili kufikisha ujumbe kwa umma kwamba sikubaliani hata kidogo na baadhi ya mambo yanavyoamuliwa katika kamati na kisha Baraza.

-          Kwa kuzingatia yote hayo nikiongozwa na kiapo naomba nianze kwa kutaja mambo nitakayozungumza nanyi, yaliyonisukuma kuwaita ili kuweka uwazi huu kwa wakazi wa Shinyanga na wakazi wa Ndembezi. Mambo hayo yatahusu:-
i.             Greda aina TEREX T180 mali ya Halmashauri Manispaa ya Shinyanga.
ii.            Hoja za barabara za lami mjini.
iii.           Hoja kuhusu JASCO.
iv.           Udanganyifu wa Bajeti 2016/17 ulioanzishwa na Baraza la madiwani na uliowasilishwa wizarani.
v.            Ujenzi wa nyumba za ghorofa mjini kati na usimamizi wake.

I.            Hoja kuhusu Greda.
Mnamo tarehe 15/06/2016 katika kikao cha kamati ya fedha nilianza kuhoji mambo muhimu kuhusiana na suala zima la maamuzi kuhusu Greda la Halmashauri aina ya TEREX ambalo limeonesha uwezo mdogo wa kutenda kazi tangu lifike manispaa tarehe 20/03/2016. Nilijenga hoja za kina baada ya kupokea taarifa za ukaguzi CAG (Exit Meet ya mwezi May 2016).

Katika kikao hicho kilipelekea kikao cha kamati ya fedha kilichofuatia kutoa hoja ya kuunda kamati ndogo ya wataalamu na madiwani nikiongozwa na barua iliyosomwa kwetu na mtunza hazina wa manispaa ikinukuu barua toka kwa RAS (Katibu Tawala Mkoa) yenye Kumb. Na. AD25/290/01A/49 ikiwa na rejea yenye Kumb. Na. AG.26/522/01/81 ya tarehe 25/04/2016 toka OR.TAMISEMI ikitoa maelekezo saba (Rejea maelekezo hayo).

Nilitafakari maelekezo hayo ya msingi yenye lengo la kujenga nidhamu katika halmashauri katika utendaji kazi, ili kutimiza maelekezo hayo nilianza kufuatilia hoja za ukaguzi kwa kina na nikataka kujua yafuatayo:-
1.    Kwa nini TEMESA walikagua Greda hilo lilipofika na kuliona lina vigezo vyote (Specifications) vya kitaalamu na baada ya kulifanyia majaribio kwa vitendo likabainika halina nguvu na uwezo wa kufanya kazi” (Hoja ukaguzi) na kisha baadae kupelekea kutofanya kazi kabisa tangu lilipofanyiwa majaribio, ingawa mratibu wa mradi wa ULGSP na mwendeshaji wa mtambo huu, walitoa maelezo kwa wakaguzi kwamba kifaa cha utambuzi wa mafuta (Fuel Sensor) hakifanyi kazi vizuri.

2.    Nilitaka kujua kwa nini wahusika (wasimamizi) wamueleze mkaguzi kwamba mtambo upo ndani ya muda wa matazamia kwa rejea kiambatisho na 04 (sikukiona) na bado hawawajibiki kumtaarifu mzabuni kulitengeneza mpaka linakutwa na hoja za ukaguzi?

3.    Nilitaka kujua Ndugu Razaro Madanka na Martin Musa ambao tayari wameshalipiwa gharama ya mafunzo na Halmashauri ya kuendesha Greda hilo Tshs. 1,050,000/= kwa hati ya malipo Na. 4/3 ya tarehe 02/03/2016 walienda kusoma au la?

4.    Nilitaka kujua mkataba unasemaje wa manunuzi ya Greda hilo.

Lakini nilitoa hoja ya Greda kurudishwa kwa kuzingatia Greda limo ndani ya muda wa matazamio na wakati huohuo kuendelea na uchunguzi wa yote hayo baada ya kuunda kamati.

Mkurugenzi alipinga na kushawishi kikao kikubali kazi ya uchunguzi wapelekewe TAKUKURU, alisisitiza wao wana wataalamu wote wakiwemo manunuzi, wahandisi wanasheria na wengineo, hivyo uchunguzi utakuwa na ufanisi mkubwa kwa TAKUKURU.

Taarifa ya TAKUKURU iliyokuja ilionesha mtambo umeharibiwa na operator na hivyo litengenezwe tu. Halmashauri nayo ikasimamia hapo bila kuangalia maeneo mengine, ambayo yanadosari zinazopaswa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kama barua toka OR TAMISEMI inavyoelekeza.

Mfano :- katika kikao  kimoja cha kamati ya fedha –mratibu wa mradi wa ULAGSP alileta hoja akiomba idhini ya kukodi wataalamu waendeshe mitambo ili huyu wakwetu apate uzoefu na sio kumkabidhi kuliendesha ,kikao kilimruhusu na akawaleta na wakawa wanalipwa posho hadi kuliharibu na kupaki kabisa.Swali ni kweli hao walikuwa wataalamu  au alikidanganya kikao  na kama ndiyo nani kaisababishia na  hasara hiyo Halimashauri? (payment voucher ni ushahidi wa kukodi ina OPARATOR) kama si muhitasari alitoa hoja ya kuhusu kulikodisha na tulikataa
-          Haitoshi katika matengenezo yamekua yamekuwa yakifanyika bila kuzingatia taratibu za TEMESA

Mfano:- Kubadili wembe wa pili tangu lije, ulifanyika kienyeji tu na kibaya zaidi spare zinazotolewa (chakavu) hazipelekwi stoo ambako ndipo mahala zinazopaswa kutunzwa hadi halmashauri itakapoamua vinginevyo, ( DISPORSAL).
-          Utata mwingine nilioubaini ni malipo yaliyofanyika tarehe 18/03/2016 ya Ths. 1,275,580 kwa L.P.O No 2015/108 iliolipwa na Halmashauri ndani ya muda wa matazamio. Sielewi idhini ilitoka wapi ya kukiuka mkataba na kuitia hasara Halmashauri bila sababu  bali UZEMBE.

Ndugu wana habari mimi niliona vyema nikamuona DC na kumueleza utata huu na nikafanya hivyo siku ya tarehe 20/11/2016. Tarehe 21 kulikuwa na baraza maalumu la kujadili  hatma ya Greda, mimi sikwenda kwa makusudi kwani nilijua uamuzi utakaotolewa ni tofauti na ninavyoelewa ukweli ulivyo,na ikawa hivyo hoja ikafungwa na baraza hilo bila  hatua yeyote dhidi ya yeyote tofauti na barua toka OR-TAMISEMI iliyoeleza .Hoja ikasimamiwa ya ushauri wa TAKUKURU tu litengenezwe na kwa kuwa limetengenezwa likathibitishwa linafanya kazi  na madiwani kupitia kazi zililizofayika katika kata zao kwa upande wangu bado naamini hoja za CAG kwa uthibitisho wa taarifa hizi za kazi baada ya matengenezo kuelekea mapokezi ya mwenge, (rejea taarifa) greda siku 4 kuchonga Km 4.3 si sawa na ni dalili  tosha  ya kwamba bado  greda halina uwezo wa kufanya kazi  IPASAVYO, liko (very slow) taratibu sana, sielewi kwa nini linatetewa, kata ya NDEMBEZI na kwingineko kabla ya mwenge kuja  limefanya kazi inayothibitisha na kutokuwa na uwezo bado. Binafsi bado naona GIZA juu ya TIJA ILIOTARAJIWA na wakazi wa manispaa ya Shinyanga katika utendaji kazi wa mtambo huo, siungi mkono maamuzi baridi ya baraza la tarehe 21/11/2016 japo taratibu za vikao tayari zimefanyika na muamuliwa na wengi na LIMEPITA.

II.         Hoja  kuhusu barabara za lami mjini
a)          ONION ROAD kudaiwa inaurefu wa  Km 1.6 wakati halisi ni Km 0.3, Boma road Km 1.6 halisi ni Km 0.3, gorverment Km 4 wakati hasi ni Km 0.7, Nyerere Km 1.1 wakati halisi ni Km 0.3 na kipande kingine kujengwa na mkandarasi  tofauti, Kenyata  Road Km 2 halisi ni Km 1.75 na Swyneton Km 2.2 halisi ni Km 1.9 ni hoja ambayo ni ya udanganyifu mkubwa  ambao niliubaini katika mkataba mmoja wa kazi aliopewa kampuni ya STEGILE kutengeneza barabarara hizo na nikagoma kusaini mkataba  mpaka nilipoomba msaada kwa katibu tawala wakati  huo (Mzee Talimo, sasa ni mstaafu) ambae alitumia wahandisi wake kufuatilia nami nilishiriki  kuwaonesha. Yalitoka maelekezo ya nini kifanyike ikiwa ni pamoja na kuacha kuripoti udanganyifu huo.

b)         Inasikitisha kuona bado udanganyifu unaendelea kwa ushahidi wa majibu ya ofisi ya mhandisi wa manispaa (rejea taarifa yao). Msimamizi mkuu wa udanganyifu huu anapaswa kuchunguzwa ajulikane achukuliwe hatua ili kujenga nidhamu katika utendaji kazi za halmashauri.

III.       Hoja kuhusu JASCO.
Mkandarasi anaejenga barabara za lami Km. 13 Manispaa, hapa kuna tatizo kubwa la mkataba kufungwa bila kuzingatia memoranda World Bank ambayo flow ya kuletewa hela itazingatia (performance Base) hali ya ufanisi katika utendaji kazi ajabu mkataba ukafungwa wa mwaka 1 (mmoja) wakati mleta fedha hajui hilo. Dosari zipo za kizembe ambazo nazo zinanipa giza pamoja na jitihada zinazoendelea kuweka mambo sawa.

IV.        Udanganyifu wa Bajeti 2016/27 upande wa ujenzi – Barabara.
Tulipokea mrejesho wa bajeti ya 2016/17 na nilipoipitia kwa kina nikagundua kilichowasilishwa ni tofauti na baraza lilivyopitisha kupitia mkutano wake. Mfano barabara ya Boma, Onion, Government, Nyerere, Swyneton hatukuzipitisha lakini zimekuja katika utekelezaji wa kazi. Inaonesha ipo hujuma ya kuwasilisha bajeti tofauti kwa matakwa ya mtu na sio baraza jambo ambalo si jema kwa maendeleo ya halmashauri.

V.           Ujenzi wa nyumba za ghorofa mjini kati.
Sheria hii haitekelezeki na itakapo kuja kusimamiwa basi athari zake ni kubwa sana. Ni sheria ambayo nimekua nikiifuatilia nikiwa Naibu Meya na sikufanikiwa kwa kukosa ushirikiano. Mtazamo wangu ni vema zikaachwa kabisa kwa eneo la mjini kati ili kutoa uonevu vinginevyo ili haki ya sheria itendeke, nyumba za kubomoa ni nyingi sana. Hili ni la mbunge au wabunge kusaidia kuweka sawa sheria hii isiotekelezeka kwa baadhi ya miji hasa Shinyanga manispaa ili watu wote wajenge nyumba imara na si maghorofa na mbadala wake maghorofa yaanze kujengwa sehemu nyingine ambako kuna maeneo yaliyo wazi.

Ndugu zangu wanahabari, nieleweke mimi ni kiongozi mwakilishi wa wananchi walionituma kusimamia maendeleo yao, hivyo na wao kupata habari ni haki yao na wajibu kama ilivyo na inavyosisitizwa katika kufanya mikutano ya wananchi ili kiongozi kuzungumza nao yanayohusu maendeleo yao. Kumbe kuongea nanyi nimewatendea haki kuwaeleza ukweli niujuavyo kuhusu nambo yote niliyoyataja. Cheo ni dhamana, naheshimu kiapo changu, hivyo kujiuzuru ujumbe wa kamati ya fedha si kosa bali ni njia ya kufikisha ujumbe kwa mambo ambayo sikubaliani nayo, na ambayo bila kufanya hivi nami nitasomeka naunga mkono kwa mujibu wa taraibu za uendeshaji wa vikao.

Ahsanteni kwa kunisikikiliza.


……………………………
DAVID M. NKULILA
DIWANI KATA YA NDEMBEZI
MANISPAA YA SHINYANGA.

Mheshimiwa David Nkulila akizungumza na waandishi wa habari leo 
Waandishi wa habari wakiendelea kuchukua matukio
Waandishi wa habari wakifuatilia hoja za mheshimiwa David Nkulila
Mheshimiwa David Nkulila akionesha nyaraka muhimu alizokuwa nazo
Waandishi wa habari wakitafakari
Waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini
Mheshimiwa Nkulila akizungumza na waandishi wa habari
Waandishi wa habari wakiendelea kuchukua matukio
Greda lililozua utata (picha kutoka maktaba ya Malunde1 blog

Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

ANGALIA PICHA- MTAMBO WA KUCHONGEA BARABARA "GREDA" UKIKABIDHIWA MANISPAA YA SHINYANGA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527