JINSI WABUNGE WALIVYOVUTANA WAKATI WA KUPITISHA MUSWADA WA HUDUMA ZA HABARI 2016



PAMOJA na Bunge kupitisha Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, wabunge kabla ya hatua hiyo waliujadili muswada huo kwa siku mbili na kutofautiana huku wengi wakionekana kuukubali.

Wabunge juzi na jana asubuhi wakiujadili muswada huo, baadhi walisema umekuja kufifisha tasnia hiyo na wengi waliukubali lakini walitaka mambo kadhaa yaboreshwe ikiwemo kuonesha bayana namna maslahi ya waandishi yatakavyolindwa na sheria hiyo.

Walisema kwa nyakati tofauti kuwa waandishi wengi wanakopwa na waajiri wao, hawalipwi na wakilipwa ni ujira mdogo na wameshindwa kupaza sauti zao wakiogopa kufukuzwa kazi huku kukiwepo na asilimia 60 ya waandishi ambao hawajaajiriwa na hakuna wa kuwasemea isipokuwa sheria hiyo.

Muswada huo uliwasilishwa juzi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ukiwa na vifungu 62 lakini jana ulipitishwa na Bunge kuwa sheria ukiwa na vifungu 67 na maboresho katika zaidi ya vifungu 30 yaliyozingatia maoni ya wabunge.

Katika majadiliano, wabunge walishauri baadhi ya vifungu virekebishwe zaidi kikiwemo kifungu cha 56 (cha awali) kinachoipa Polisi mamlaka ya kutwaa kifaa chochote cha chombo cha habari kama kimekwenda kinyume cha sheria na kutaka madaraka hayo yarejeshwe kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) alisema muswada huo umekuja kuibana sekta ya habari kwa kuzuia watu wenye ujuzi wa kuandika kuzuiwa kufanywa hivyo kwa kuwekewa vikwazo vya elimu ya uandishi na Bodi ya Ithibati.

Zitto alisema uandishi wa habari ni kazi ya wito akitumia neno ‘passion’ na si vyema ikawekewa vigezo vya udhibiti kama wanasheria, madaktari na wahasibu kwa kuwa wako watu katika historia hawakuwa na elimu ya uandishi lakini ni waandishi wa kuigwa nchini na duniani.

Alimtolea mfano Mbaraka Islam ambaye alitoa taarifa za kuzama kwa meli ya Mv Bukoba mwaka 1996 bila kuwa na taaluma ya habari na sasa ni mwandishi wa mfano. Pia Zitto alimgusia Dk Harrison Mwakyembe (sasa Waziri wa Katiba na Sheria) ambaye alianza kazi ya uandishi wa habari bila kusomea na sasa ni mwanasheria mzuri nchini.

Kwa upande wake, Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajabu (CCM) aliunga mkono muswada hasa maeneo yanayozungumzia mwandishi kukatiwa bima na kuwepo kwa Mfuko wa Habari utakaohusika kufadhili waandishi kusoma kozi fupi na ndefu.

Adadi, alisema waandishi wa habari wanafanywa kama vibarua na baadhi ya wamiliki na wanakosa haki zao. Alisema nusu ya waandishi hawalipwi wala hawana barua za ajira na wanaogopa kutoa taarifa, wanaogopa kufukuzwa kazi.

Pamoja na hilo, Adadi aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kabla ya kuwa Balozi wa Tanzania, Zimbabwe, alisema kuna watu wanang’ang’ana kuwa muswada huo ni mbaya ili kuzuia waandishi wa habari wasipate haki zao.

Adadi alitaka muswada ulinde maslahi ya waandishi wa habari wazawa na wageni na kuunga mkono uwekezaji wa asilimia 49 wa vyombo vya habari kwa raia wa kigeni nchini dhidi ya asilimia 51 ya wazawa na kutaka wabunge wajue hakuna sheria isiyompa waziri mamlaka ya kusimamia mambo fulani kwa mujibu wa kanuni.

“Nashauri madaraka ya Mkurugenzi wa Mashitaka yarejeshwe badala ya kuachia Polisi kuchukua hatua ya mambo yote yanayohusika na uchochezi,” alisisitiza Adadi.

Naye Mbunge wa Mafinga, Cosato Chumi (CCM) ambaye kitaaluma ni mwandishi, alishauri muswada uzungumzie asilimia 60 ya waandishi (correspondent) wanaofanyakazi kwa maslahi duni na kutaka utetee maslahi ya waandishi kulipwa na kutonyanyaswa na wamiliki wa vyombo vya habari.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) yeye alishauri kipengele kinachowanyima waandishi uhuru wa kupata habari kutoka vyanzo mbalimbali kifutwe kwa kuwa kinaminya uhuru wa habari Kikatiba.

“Kipengele namba 20 kifungu kidogo cha tatu kifutwe kabisa ni kibaya. Naipongeza serikali kwa kufuta kifungu namba 50 (4) naomba na kipengele cha nane nacho kiondolewe kabisa,” alisema Bashe.

Akichangia, Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema) alisema atapeleka marekebisho katika muswada huo kutokana na kutokubaliana na mambo kadhaa na kutaja miongoni mwake kupinga wanahabari kuwa na mavazi maalumu na kuzuiwa wageni kumiliki asilimia 100 ya hisa kwenye chombo cha habari.

Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM) alisema tasnia ya habari haijawahi kupata heshima inayostahili kwa wanahabari na wamiliki wa chombo cha habari lakini muswada huo sasa utawapa heshima hiyo kutokana na mageuzi yaliyofanywa ili wanahabari wawe na hadhi kama ilivyo kwa wahandisi na madaktari.

“Nahisi wabunge wa upinzani mnataka uandishi wa habari uwe kama shule ya chekechea na usifike chuo kikuu...,” alisema.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Mmasi (CCM) alimtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape kuweka kwenye kanuni mambo yanayofaa kuandikwa na yasiyofaa kuandikwa kwenye vyombo binafsi vya habari ili kuepuka mambo yasiyofaa kwenye tamaduni za kitanzania.

Kwa upande wa Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya Salum (CCM) alisema Mfuko wa Mafunzo wa kuendeleza wanahabari utengewe fedha haraka na pia wanahabari wa vyombo binafsi wapate nafasi ya kusaidiwa na mfuko huo kwenye mafunzo.

Sheria hiyo inasubiri saini ya Rais John Magufuli ianze kutumika baada ya kutungwa kwa kanuni na Bunge kuridhia. Tayari Rais akizungumza na waandishi wa habari juzi, alisema atasaini sheria hiyo siku hiyo hiyo itakapowasilishwa mezani kwake.

Imeandikwa na Gloria Tesha-HabarileoDodoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post