IDADI YA WATU WALIOFARIKI AJALI YA NOAH,LORI SHINYANGA YAFIKIA 19


Idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya gari ndogo Toyota Noah yenye namba za usajili T 232 BQR imefikia 19 baada ya majeruhi mmoja kufariki dunia.Mtoto huyo amefariki dunia majira ya saa mbili usiku Novemba 07,2016 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.


Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Daniel Maguja alisema ,majeruhi aliyefariki ni mtoto anayeitwa Hamisa Matiko Ali mwenye umri wa miaka mitano ambaye hali yake ilibadilika ghafla na kufariki majira ya saa mbili usiku.


Dkt. Maguja alisema majeruhi mwingine Salima Kiza mwenye umri wa mwaka mmoja ambaye alivunjika mfupa wa paja la kushoto alipewa rufaa ya kwenda kutibiwa hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza na kwamba majeruhi Boniface Richard anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.


“Katika maiti zote 19 zimeshatambuliwa na ndugu zao wamefika kuchukua mwili kwa ajili ya taratibu za mazishi",alisema.


Kwa upande wake mama mkubwa wa marehemu Amina Katigile alisema walipata taarifa za ajali hiyo na kufuatilia ambapo alikuta mdogo wake Debora Mayingu,ambaye alikuwa kwenye gari hilo amefariki dunia na watoto wake wawili wamejeruhiwa.


Alisema mtoto Hamisa Matiko Ali aliyefariki alikuwa na mama yake Debora Mayingu kwenye gari hilo pamoja na mtoto mwingine Salima Kiiza(01) ambaye amepelekwa Bugando kwa ajili ya matibabu.


“Hatuna la kufanya bali tunamuachia mungu kwa kuwa ndiye anayempanga na muweza wa yote, mtoto Hamisa Matiko aliyefariki mimi ni mama yake mkubwa,na tumefika hapa kuchukua mwili kwa ajili ya taratibu za mazishi, tunamuomba mungu amsaidie mtoto aliyepewa rufaa kwenda Bugando apate nafuu “alisema Katigile.


Ajali hiyo ilitokea NovembA sita mwaka huu majira ya saa 1.30 usiku katika kijiji cha Nsalala kata ya Tinde wilaya ya Shinyanga wakati gari hilo aina ya Noah lilipokuwa likitoka Nzega kuelekea Tinde liligongana uso kwa uso na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T198CDQ na tela lake lenye namba T283CBG.


Gari aina ya Noah ilikuwa ikiendeshwa na Seif Muhamed (32)mkazi wa Tinde huku lori lilikuwa likiendeshwa na Aloyce Kavishe(46)mkazi wa Dar es salaam, ambapo wote wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kwa hatua zaidi za kisheria kuhusiana na ajali hiyo iliyopoteza maisha ya watu 19.


Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post