BAADA YA UKUTA KUYEYUKA, CHADEMA YAIBUKA NA OPERESHENI YA 'KATA FUNUA'



Baada ya kuanzisha na hatimaye kukwama kuitekeleza operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), Chadema imekuja na nyingine itakayokwenda kwa jina la ‘Kata Funua’.



Operesheni hiyo mpya imetangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ikilenga kukipa chama hicho mafanikio katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na ule mkuu ujao.


Mbowe amesema hayo katika kikao cha uchaguzi wa mwenyekiti wa kanda wilayani Masasi mkoani Mtwara.


“Kiongozi yeyote atakayeonyesha nia ya kutukwamisha hatutamvumilia, tutamuondoa ili tuweze kuendelea na safari yetu na kumaliza kutembelea kanda zote,” amesema.


Amesema ziara hizo ndizo zitakazoipa nafasi chama hicho kuchukua maeneo mengi zaidi hasa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019.


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema umoja na mshikamano ndiyo msingi imara utakaowasaidia kuweza kufikia malengo.


“Ili kufanikiwa lazima kuwe na umoja imara baina ya viongozi wa chama. Mtu yeyote atakayekuwa na nia mbaya na umoja huu achukuliwe hatua mara moja ili kuepuka kutokea kwa migogoro,” amesema.


Naibu Katibu Mkuu wa Chadema – Zanzibar, Salum Mwalimu amemshukuru Rais John Magufuli kwa kukipa fursa adhimu chama hicho kutokana na kuzuia mikutano ya kisiasa majukwaani jambo ambalo limewasaidia kujipanga vizuri katika uchaguzi ujao.


“Safari hii ni fursa kwetu, tumejipanga kiuhakika na si kwa kubahatisha tunapoelekea katika uchaguzi wa serikali za vijiji, vitongoji, mitaa mwaka 2019 na baadaye uchaguzi wa wabunge na Rais ifikapo 2020,”amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post