JELA MIAKA MIWILI KWA KUJIFANYA USALAMA WA TAIFA

Mahakama  ya Wilaya ya Ilala imemhukumu Seleman Manoti, kifungo cha miaka miwili jela kwa kupatikana na hatia ya kujifanya usalama wa Taifa.

Hata hivyo, mahakama imetoa hukumu hiyo bila mshitakiwa kuwepo mahakamani kutokana na kuruka dhamana kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Flora Haule alisema kuwa upande wa mashitaka, ulileta mashahidi wanne kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma hizo.

Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imeridhishwa na ushahidi huo na kwamba mahakama inamtia hatiani mshitakiwa licha ya yeye kutokuwepo.

“Hati ya kumkamata mshitakiwa itolewe na adhabu hii itaanza kutumika pindi mshitakiwa atakapokamatwa kwani alitoroka akiwa na haki ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Haule.

Wakili wa Serikali, Ester Kyara aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa wengine.

Inadaiwa kuwa Novemba 19, 2014 maeneo ya Kariakoo Msimbazi wilayani Ilala, mshitakiwa alijitambulisha kwa Issaya Odelo na Charles Odinga kuwa Ofisa Usalama wa Taifa, kitu ambacho alijua si kweli. 

Katika hatua nyingine, kondakta Ally Salum (23), mkazi wa Mwananyamala, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kuiba daladala.

Mbali na mshitakiwa huyo, Exavery Kaunga (44) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Kiwalani, Minazi Mirefu, aliachiwa baada ya ushahidi dhidi yake kuwa na shaka.

Akitoa hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan, alisema kuwa upande wa mashitaka ulileta mashahidi wanne kuthibitisha kosa hilo.

“Nimeridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, nakutia hatiani mshitakiwa kama ulivyoshitakiwa kwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela,” alisema Hakimu Hassan.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine. Hata hivyo, mshitakiwa alipoulizwa ni kwa nini asipewe adhabu kali, hakujibu chochote na mahakama kutoa adhabu hiyo.

Washitakiwa hao walishitakiwa kwa makosa mawili ya kula njama kutenda kosa ambapo inadaiwa kati ya Julai 5, mwaka jana, washitakiwa walikula njama kutenda kosa.

Pia inadaiwa Julai 5,2015 pembezoni mwa barabara ya Nyerere katika Kituo cha Mafuta cha Victoria, washitakiwa waliiba gari lenye namba za usajili T 624 CSH aina ya Eicher mali ya Kampuni ya White Swan.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post