MBUNGE GODBLESS LEMA ASWEKWA RUMANDE KWA UCHOCHEZI KATIKA MITANDAO YA KIJAMII



MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema ameswekwa rumande na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa tuhuma za kusambaza maneno ya uchochezi katika mitandao ya kijamii usiku wa kuamkia jana.

Lema alikamatwa na polisi alfajiri nyumbani kwake kata ya Engutoto Njiro ndani ya Jiji la Arusha akiwa bado hajaamka.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo alikiri polisi kumsweka rumande mbunge huyo na kusema kuwa inamhoji na kufahamu ni kwa nini alisambaza maneno ya uchochezi yenye lengo la kuvunja amani ya nchi. Alisema Lema alikamatwa saa 12 asubuhi nyumbani kwake Njiro akiwa bado amelala.

Alisema baadhi ya maneno hayo ni “Kama mauti imepoteza utukufu wake hakuna statement ya kurudisha nyuma Arusha kuandamana.”

Kwa mujibu wa Kamanda, maneno hayo aliyoyatoa Lema ni ya uchochezi na kuvuruga amani ya nchi na ndiyo maana wanamshikilia kwa mahojiano juu ya kauli zake hizo.

Alisema Watanzania wanatambua umuhimu wa amani na hakuna mtu aliye juu ya sheria, hivyo ni vyema wakaheshimu amani na utulivu uliopo.

Aidha, alisema utii wa sheria bila shurti ni vyema ukazingatiwa ili kuepuka machafuko ambayo yanaweza kutokea kutokana na maneno hayo ya uchochezi.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527