Shamba La Waziri Lavamiwa Na Watu Wasiojulikana...Wakata kata Mikarafuu,Minazi na MihogoSHAMBA la mikarafuu , minazi pamoja na mihogo la Waziri asiye na wizara maalumu Zanzibar Said Soud Said limevamiwa na kuhujumiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia June 14 mwaka huu .


Katika hujuma hizo zilizotokea katika shamba lililoko Mgelema Jimbo la Chonga Wilaya ya Chake Chake , jumla ya mikarafuu 29 , minazi 16 pamoja na mashina 250 ya muhogo yamengo’lewa na baadhi ya mengine kufyekwa na kitu chenye ncha kali .

Katika tukio hilo mikarafuu michanga 15 imeng’olewa na kutupwa ndani ya shamba , na mengine 14 iliyokuwa tayari kuzaa imekatwa na kuachwa ndani ya shamba .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi , Said Soud Said alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinafanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika na vitendo hivyo vya kuhujumu mazao makuu ya uchumi wa nchi .

Aidha alieleza kwamba , baadhi ya wananchi wanalichukulia suala la siasa kama ni chuki au fitina , na kuwashangaa wanaoendesha humuma hizo kwani haziwezi kusaidia kutatua changamoto za kisiasa .

“Ni jambo la akushangaza kuona mikarafuu , minazi pamoja na mihogo inafanyiwa hujuma namna hii , ni vyema vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili wausika wapatikane na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ”alisisitiza.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mwanajuma Majid Abdalla akizungumza katika eneo la tukio alisema Serikali imejapanga vyema kukabiliana na vitendo vya hujuma na kuwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi kufanikisha kukamatwa kwa wahusika wa vitendo hivyo .

Alisema kwamba Serikali inategemea zao la Karafuu pamoja na minazi kwa ajili ya kukuza uchumi wake , na kwamba kitendo cha kukatwa kwa mikarafuu sio tu kwamba kinarudisha nyumba maendeleo ya mwananchi bali pia na Taifa kwa ujumla .

“Matendo haya kwa kweli sio kama yanaathari kwa mwenye shamba pekee , bali hta uchumi wa Nchi unaathirika kwani Serikali inategemea sana zao la karafuu kupata fedha za kigeni ”alieleza .

Kwa upande wake kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba Shekhan Mohammed Shekhan ameahidi kwamba askari wataendesha doria na msako wa kuwasaka wahusika ili waweze kufikishwa kwenye mahakamani .

Alisema kwamba katika msako huo , watawatumia askari Shehia , Polisi jamii pamoja na wananchi wa kawaida na kuongeza kuwa watakaobainika watachukuliwa hatua hata kama watakuwa nje ya Mkoa huo .

Kwa hili hatutakuwa na huruma na mtu , tutafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za jeshi ,pia tutawatumia askari shehia , polisi jamii pamoja na raia wema abao wamekuwa wakitupa taarifa ”alisisitiza .

Hivyo Kamanda shekhan amewataka wananchi kutotumia fursa hiyo kutoa taarifa ambazo sio sahihi na ambazo zinawahusu wananchi wenye chuki binafsi. Na kwamba jeshi la polisi litazifanyia uchunguzi taarifa hizo kabla ya kuzichukulia hatua .

Matendo ya hujuma kwa baadhi ya mali za wananchi yanaendelea kutokea katika mikoa ya Pemba baada ya kumalizika uchaguzi Mkuu wa marejeo uliofanyika machi 20 mwaka 2016 yakihusishwa na itikadi za kisiasa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post