Spika : Kuna Wabunge Wanaingia Bungeni Wakiwa Wametumia Bangi,Viroba na UngaKama unashangaa kusikia kwamba aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, ametimuliwa kwa kuingia bungeni akiwa amelewa.
Bila shaka utachoka zaidi ukisikia kuna wabunge kadhaa huingia kwenye ukumbi wa Bunge wakiwa wametumia vilevi vikali zaidi vikiwamo bangi, viroba na dawa za kulevya.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, ndiye aliyefichua siri hiyo jana.
 
Kutokana na hali hiyo, Ndugai alisema sasa wanafikiria kuweka vifaa maalumu vya kupima ulevi kwa watunga sheria hao na kutafuta wataalamu wa ushauri nasaha watakaowapa msaada wa kisaikolojia.

“Kikubwa tunataka kuweka mkakati wa kujaribu kumtambua (mbunge) mmoja mmoja na kujaribu kuwatafuta wale watu wanaotoa ushauri nasaha au watu wa mambo ya saikolojia.

“Tunajaribu ku-identify (kuwatambua) watu maalum wanaoweza kutusaidia kuzungumza na hawa watu ili waondokane na matatizo yale ambayo tutaweza kuyagundua… lakini wale wanaofanya kwa kificho itakuwa tabu kidogo. Lakini huko mbele tutakwenda kwenye vifaa,” alisema Ndugai na kuongeza:

“Maana siyo ulevi tu, kuna sigara kubwa (bangi), unga (dawa za kulevya)… watu wanapiga konyagi hadi mchana, kimsingi mambo ni mengi,” alisema Ndugai.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kwa taarifa hiyo asieleweke vibaya kuwa ni wabunge wote hutumia vilevi kabla ya kuingia bungeni, bali wapo wachache wenye kawaida hiyo na kwamba hao ndiyo wanaostahili kusaidiwa na wataalamu wa saikolojia na pia kufunga vifaa maalum vya kuwabaini.

“Simaanishi wote (wabunge), maana mtu anaweza kufikiri ni wabunge wote… hapana. Hili ni kundi dogo mno la wabunge (na) hawajai hata mkononi. Lakini wabunge walio wengi ndiyo wazuri sana, hawanywi pombe wala nini. Kikundi hiki kinahitaji msaada wa ushauri,” alisema.

Akiendelea kufafanua, Ndugai alisema: “Tatizo ni kubwa kiasi… na siyo la kulewa peke yake, lazima kuangalia namna gani ya kumbana mtu yeyote ambaye amelewa, (kama) ametumia madawa ya kulevya.

“Kwa hiyo linatakiwa suala la kubadili kanuni litazamwe kwa mapana, siyo leo unadhibiti aliyelewa, kesho unadhibiti hali hii… ni lazima kuliangalia (suala hili) kwa mapana yake,” alisema Ndugai.

Alisema tofauti na kikao cha asubuhi ambacho ndicho Kitwanga aliingia akiwa amelewa (Ijumaa Mei 20, 2016), kile cha jioni ndiyo huwa kibaya zaidi.

“Nakubaliana ipo haja ya kuwa na vifaa, hasa bunge la mchana ndiyo huwa (na tatizo) zaidi, maana kuna baadhi ya wabunge wanakuja pale mchana wameshalewa,” alisema.

Alisema wabunge hao ambao huingia bungeni wakiwa wameutwika, kubwia unga ama bangi, wakati mwingine hutibua vikao vya Bunge.

“Huyo mbunge mmoja au wawili, wanaweza kutibua Bunge …ukajikuta Bunge zima linatibuka kumbe wenzenu hawapo `normal’ (kawaida). Kwa hiyo tunaendelea kuangalia (namna ya kudhibiti hali hiyo) kwa kupewa mawazo na Watanzania,” alisema Ndugai.

Alisema wakati mwingine Kamati ya Bunge ya Maadili inakaa na kufanya maazimio juu ya mbunge fulani, kumbe ukweli ni kwamba mhusika hakuwa sawa wakati akifanya tukio hilo la kukiuka kanuni bali anakabiliwa na msukumo ‘fulani’.

Akieleza kuhusu hatua watakazozichukua dhidi ya Kitwanga ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Ndugai alisema hawafikirii kumpa adhabu yoyote baada ya ile ya kuondolewa uwaziri.

“Kuhusu Kitwanga, hatuwezi kumchukulia hatua yoyote ile. Kama ni mlevi sana, anatakiwa kufanyiwa `counseling’ (kupewa ushauri nasaha) ili kuondokana na hilo tatizo. Mimi siwezi kujiunga na wale ambao wanamsakama, mimi ni baba na mama wa wabunge wote… kwa yule ambaye ameteleza, mimi ni wajibu wangu kumrudisha kwenye mstari. Ndiyo kazi nitakayofanya.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post