Waziri Nape Awakingia Kifua Maafisa Habari Na Waandishi wa Habari
Kukosekana kwa maafisa habari katika halmashauri nyingi nchini na waliopo kutoshirikishwa kwenye vikao vya maamuzi imetajwa kuwa ni changamoto kubwa, ambayo imekuwa ikisababisha waandishi wa habari kushindwa kupata taarifa za shughuli mbalimbali zinazofanywa na serikali na kuwepo urasmu mkubwa.Hayo yalielezwa juzi na waziri wa habari utamaduni sanaa na michezo Nape Nnauye wakati akizungumza na waandishi wa habari, maafisa utamadunia,wasanii,maafisa habari na wadau wa michezo mkoani Shinyanga ambapo aliwataka watendaji wa serikali kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari huku akiwaonya wanaotoa vitisho kwa waandishi wa habari.


Waziri alisema kutokuwepo kwa maafisa habari katika halmashauri za wilaya na kutoshirikishwa kwenye vikao vya maamuzi bado ni changamoto kubwa na kuagiza halmashauri zote kuhakikisha zinakuwa na maafisa habari.


“Tunataka kila halmashauri iajiri maafisa habari na watengewe idara yao na waruhusiwe kuingia kwenye vikao vya maamuzi,tunataka nchi ijazwe na habari,hawa ni daraja zuri kati ya waandishi wa habari,serikali na wananchi,na tunataka maafisa habari wa kuajiriwa siyo wa kukaimu nafasi”,alisema Nape.Nape alisema tatizo lililopo ni ukiritimba mkubwa katika kuajiri maafisa habari na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo. 

Alisema kutokana na maafisa habari kutoshirikishwa kwenye vikao vya maamuzi inapofikia hatua ya waandishi wa habari kutaka habari inakuwa kama vita kwani maafisa hao wanakuwa hawana cha kuongea kutokana na kukosa taarifa muhimu. 

“Leo hawa maafisa habari hawaingii kwenye vikao vya maamuzi ,mwandishi wa habari hata upige kelele namna gani hawawezi kutoa taarifa maana hawajui watazungumza nini sasa, tunataka wawe na sauti maana wao ndiyo wanayoiunganisha halmashauri na wananchi hata kama kuna jambo limetokea tofauti wanatoa taarifa”,alisema waziri. 

Waziri huyo wa habari aliwatahadharisha wat baadhi ya watendaji wa serikali wanaokataa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari na kuwanyima uhuru wa kuipasha habari jamii kuacha tabia hiyo mara moja kwani inawanyika haki ya kupata habari wananchi. 

“Tutahakikisha tunalinda uhuru wa vyombo vya habari,tunataka watendaji wa serikali watimize wajibu wao,lakini pia waandishi wa habari mzingatie maadili ya kazi yenu”,aliongeza Nape. 

Awali wake mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Kadama Malunde akitoa taarifa ya Klabu kwa waziri ,alisema changamoto kubwa iliyopo, ni baadhi ya watendaji kwenye halmashauri za wilaya hawataki kuandikwa vibaya hata kama wanafanya mambo mabaya hivyo kushindwa kutoa ushirikiano kwa waandishi. 

“Kutokana na tumbua tumbua majipu iyoendelea,tumeanza kuona dalili za baadhi ya watendaji katika halmashauri za wilaya kubagua waandishi wa habari, ukionekana unaandika maovu yanayofanywa katika halmashauri basi hualikwi kushiriki katika kazi za halmashauri husika,hawataki kuandikwa vibaya hata kama wanafanya mambo mabaya”,alisema Malunde. 

Malunde alisema waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya rais John Magufuli katika kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanawajibika kwa wananchi. 


Mwenyekiti huyo wa waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga alimtaka waziri wa habari kuungana na wadau wa habari kuwakemea viongozi wenye tabia za kutotoa ushirikiano kwa waandishi wa habari,ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kubana uhuru wa vyombo vya habari na kunyanyasa waandishi wa habari. 

Naye meneja wa Radio Kahama FM Marco Mipawa alisema baadhi ya watendaji wa serikali wamekuwa wakiwachukulia hatua watendaji wa serikali wa ngazi za chini ,pindi wanapozungumzia changamoto zilizopo kwenye maeneo yao kwa vyombo vya habari na kumuomba waziri kulifanyia kazi suala hilo hilo kwani linaminya uhuru wa kupata habari na kunyanyasa watendaji hao.
Na Paul Kayanda-Malunde1 blog 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post