SERIKALI YAAGIZA WANAOMILIKI MIGODI YA MADINI YA TANZANITE BILA KUENDELEZA WARUDISHE LESENI




Serikali imeagiza wamiliki wa migodi ya madini ya tanzanite ambao migodi yao imesimama kwa muda mrefu bila uzalishaji kwa madai ya kutokuwa na madini, warudishe leseni zao wizarani mara moja.


Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prosefa James Mdoe, mara baada ya kukagua migodi ya tanzanite ya Kitalu B,D na kitalu C kinachomilikiwa na kampuni ya Tanzanite One, akiwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge inayosimamia shughuli za Wizara ya Nishati na Madini.


Profesa Mdoe alisema Sheria ya Madini ya 2010 iko wazi kwa wamiliki wa migodi ambao hawajazalisha kwa muda mrefu, kwa kuwa inataka warudishe leseni ili wapatiwe eneo lingine lenye madini.


Amesema kuendelea kusimama au kuchimba na kuingia mgodi mwingine ni kinyume na sheria na hatua kali zitachukuliwa.


Katibu Mkuu huyo alisema kuwa migogoro mingi ya wachimbaji wa tanzanite, ni ya ‘mitobozano’ kwa maana ya wachimbaji kuingia katika maeneo ya wenzao na watu kutofuata sheria zilizowekwa na Serikali kwa sasa haitavumilia.


Alisisitiza kila mchimbaji wa madini ya tanzanite wilayani Simanjiro, kuheshimu sheria ya madini iliyowekwa na Serikali badala ya kufanya kazi ya uchimbaji kwa kufuata sheria ambazo si rasmi.


‘’Mgodi wako ukimaliza uzalishaji nirudishie leseni yangu, lakini kuchimba kwa kwenda katika mgodi wa mchimbaji mwingine, ni kinyume na sheria,’’ alisema.


Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Chumbuni Zanzibar, Ussi Salumu Pondeza, alisema wataishauri Serikali kushughulikia tatizo la mtobozano mapema kabla ya mchimbaji kuingia gharama kubwa.


Alisema pia wamejifunza mambo mengi katika ziara hiyo na wana mengi ya kuishauri Serikali ili madini hayo yanufaishe nchi ya Tanzania na si nchi nyingine.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527