LOWASA APONGEZWA,MBOWE AWATAKA WATANZANIA WASIFE MOYO KWA MATOKEO YA UCHAGUZI YALIYOPINDULIWA


FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewashauri Watanzania wasife moyo kwa matokeo mabaya ya uchaguzi yaliyopinduliwa; na kwamba matokeo hayo yawe chachu ya kufanya vizuri zaidi katika uchaguzi ujao, anaandika Josephat Isango.Alisema uchaguzi si tukio, bali mchakato; na kwamba kama kuna watu wamekufa moyo kwa sababu ya kilichofanywa na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupindua matokeo, hasa ya urais, watafakari upya na wajipange kwa kazi kubwa inayokuja, kwani mafanikio ya kisiasa hayapimwi kwa tukio moja la uchaguzi na matokeo yake. Alisema matokeo hayo yanapswa kuwatia hasira na kuwahamasisha waendelee kupambana,

Mbowe amesema hayo Masaki, nyumbani kwa Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa Zamani ambaye pia alikuwa Mgombea Urais wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwenye hafla ya kumshukuru Mungu iliyoandaliwa na familia hiyo. Ukawa unaundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.

“Hatukushinda serikali kuu kama tulivyokusudia na kupenda iwe kwa sababu ambazo si wakati wake kuzisema sasa, lakini ni vema tukumbuke kwamba mapambano tunayofanya, kama kuna yeyote miongoni mwetu anafanya kwa ajili yake binafsi, ana wajibu wa kujitafakari upya,” alisema Mbowe.

Aliongeza kwamba, kazi ya mapambano wanayofanya viongozi sasa ina manufaa kwa kizazi kijacho, na kama wanaoifanya sasa wakafanikiwa kuonja matunda ya kazi ya mikono yao basi ni jambo la kumshukuru Mungu.

“Kazi anayofanya Lowassa (Baba Kadeti) si lazima aone matunda yake leo, huenda mtoto wake ataonja na asipoonja Kadeti basi wajukuu wataonja matunda hayo na kutambua mchango mzuri wa babu yao kwa kazi kubwa ya maana anayofanya sasa,” alisema.

Aliwahimiza Watanzania zaidi ya 600 waliokuwepo kwenye halfa hiyo kuwa wale walio wafuasi wa vyama vya siasa hata wasio na vyama wana wajibu wa kuendelea kwa nguvu zote na kazi ya kupambana ambayo Lowassa amejiunga nayo, kwani wakati wa uchaguzi watu wengi walipigana kumsaidia sio kwa ajili ya familia yake ila walifanya vile kwa sababu ya nchi hii huku Lowassa akiwa kiongozi na mpeperusha bendera.

Mbowe alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania waendelee kumwombea neema, ujasiri na afya njema Lowassa kwani taifa bado linamhitaji kuliko pengine anavyohitajika na familia yake.

Aidha, Mbowe alimsifu pia Regina, mke wa Lowassa, kwa ujasiri wake na familia nzima kwa uamuzi mzuri na ujasiri aliochukua katika kuhakikisha Watanzania wanatafuta haki na ujasiri kwa kukata minyororo ya watesi.

“Mama ulikuwa jasiri kwenye kampeni katikahatrua za awali, lakini baadaye ulipata ujasiri zaidi kama mgombea wetu wa urais (Lowassa) lakini baadaye ulipata ujasiri zaidi hata kuliko wanasiasa wengine, asante sana kwa kuondoa woga, asante kwa kuongoza familia na wote tuendelee na mapambano.” alihimiza Mbowe.

Kabla ya Mbowe kusimama, neno la kuwashukuru watu waliofika nyumbani lilitolewa na Regina akasema familia, hasa Lowassa mwenyewe, ilikuwa inasubiri kwa hamu siku ya kumshuruku Mungu na Watanzania kwa mazuri mengi aliyowatendea.

Hafla hiyo ya shukrani ilianzia kwa ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Azania Front, Dar es Salaam. Lilichagizwa na nyimbo kadhaa za shukrani zilizopendekezwa na Lowassa mwenyewe, na kuimbwa na washiriki wote, wakiwamo wa madhehebu mengine ya dini.

Miongoni mwa washiriki wa hafla hiyo ni baadhi ya wanachama wapya wa UKAWA waliojiengua CCM mwaka jana, wakiwamo Hamisi Mgeja, Mgana Msindai, Lawrence Masha, John Guninita, na wengine.

Ilihudhuriwa pia na wanasiasa, viongozi wa dini wa madhehembu mbalimbali, vijana na wazee, matajiri na watu wa kawaida kutoka sehemu mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali.

“Tumepata mengi mazuri, tunaweza kusafiri kwenda Monduli na kurudi si sababu tuna magari mazuri kuliko wengine; tunaweza kusafiri kwa ndege na tukarudi salama, lakin hata wakati mwingine unasikia mtu anakupigia simu kukusalimu au kukuandikia ujumbe mzuri wa faraja, haya yote ni sababu ya Mungu na tukaona leo tufike Kanisani kusema Mungu asante kwa mema yote uliyotujalia,” alisema Regina akiwa amejawa tabasamu muda wote, huku akishangiliwa.

Wajukuu wa Lowassa walijumuika kumwimbia babu yao wimbo kutoka miongoni mwa tenzi za Injili zilizoandaliwa kwa ajili hiyo, huku wakiongozwa na mpiga kinanda.

Baada ya wajukuu, Masha alitumbuiza washiriki kwa wimbo wa Kiingereza “Amazing Grace,” akatuzwa kiasi cha Tsh. 50,000 ambacho, hata hivyo, alikigawa kwa wajukuu wa Lowassa.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Lowassa aligombea urais mwenye mvuto kuliko wote, lakini aliibuka mshindi wa pili katika matokeo yenye utata, akiwa nyuma ya John Magufuli.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post