MWANAMKE ALIYEPAMBANA NA MAJAMBAZI ASIMULIA MKASA MZIMAMwanamke aliyepambana na jambazi na kufanikiwa kumnyang’anya bunduki aina ya SMG, Sophia Manguye (46), amepewa zawadi ya Sh 500,000 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Tarime/Rorya, Gemini Mushy.


Mwanamke huyo ambaye aliomba Serikali kumpa silaha ili kujilinda, alisema kuwa hajaridhika na zawadi hiyo kwa kuwa kama asingemmudu jambazi huyo watu wengi wangepoteza maisha.

Hata hivyo, Mushy alimwomba Manguye kupokea kiasi hicho japokuwa ni kidogo kwa kuwa ni zawadi kutoka ofisi yake.

Tukio hilo lilitokea Februari 9, saa 2.42 usiku, baada ya watu watatu kufika dukani kwake, mmoja wao akiwa na bunduki kisha kumwamuru atoe fedha alizokuwa nazo.

Manguye alisema alichukua Sh80,000 alizokuwa nazo na kumkabidhi jambazi huyo, lakini hakuridhika na kumlazimisha aongeze kiasi kingine.

“Nilipandwa hasira nikanyanyuka wakati jambazi anainama kuangalia kwenye kiboksi cha fedha, nikamkamata kifuani na kung’ang’ania mkanda wa bunduki, akaanza kunivuta kwenda nje, nami nikamvutia ndani, lakini alifanikiwa kunitoa nje akaniangusha chini, lakini sikuachia mkanda wa bunduki,” alisema Manguye na kuongeza:

“Aliposikia wananchi wameanza kupiga yowe akaniachia na kutoa mkanda wa silaha begani, akakimbia na kuniachia bunduki. Wakati huo huo jambazi mwingine alikuwa amekamatwa kwenye duka la Zaituni Magasi, wananchi walipofika wakaanza kumshambulia, wakati huo taarifa ilikuwa tayari imetolewa Kituo cha Polisi Sirari, wakafika kumchukua,” alisema.


Hii ni mara ya pili kwa Manguya kuvamiwa na majambazi wenye silaha, ambapo mwaka 2014 alivamiwa dukani kwake na majambazi waliokuwa na bunduki, lakini alifanikiwa kumpiga kwa kigoda aliyekuwa na bunduki na alianguka chini.

Magasi alisema wakati wa tukio hilo, alikuwa amevamiwa na majambazi waliokuwa na bunduki, mapanga na nondo.

“Wakati anatoka mvunguni mdogo wangu alimkamata kwa nyuma na kummudu huku akipiga kelele, watu wakafika wakaanza kumpiga hadi akazimia, polisi walipofika wakamwokoa kwani kidogo wamuue,” alisema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post