WAZIRI JUMANNE MAGHEMBE AMSIMAMISHA KAZI KIGOGO NA MAOFISA MISITU WOTE TANZANIA



Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Bw. Mohammed Kilongo na Maofisa wa Misitu wa Mikoa nchi nzima kupisha uchunguzi wa upotevu wa mapato ya Serikali.


Akizungumza jana na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya Wizara hiyo Dar es Salaam, Prof. Maghembe alisema agizo hilo limekuja kutokana na ubadhilifu unaofanywa na Maofisa wa ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali yanayotokana na rasilimali za misitu katika Mikoa na Wilaya kwa kutowasilishwa katika mfuko Mkuu wa Serikali.


Aliagiza pia maofisa hao wote wanaokusanya maduhuri ya Serikali katika Wilaya watumie muda wa siku kumi kuanzia jana kuhakikisha maduhuri yote yaliyokusanywa yanapelekwa benki ikiwa ni pamoja na kukabidhi vitabu vya kukusanyia mapato kinyume cha hapo watachukuliwa hatua kali za kisheria.


“Wale district forestry officers wote wapeleke vitabu vyao wanavyokusanyia maduhuri ya Serikali kwenye ofisi za Kanda, Naibu Katibu Mkuu tusaidie kuwasiliana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali ifanye ukaguzi wa vitabu hivyo ndani ya siku kumi tuhakikishe fedha zinazotakiwa zinaingia kwenye mfuko wa Serikali, Mtu anakusanya fedha ya Serikali toka mwaka 2004 mpaka leo hajapeleka benki ananeemesha hali yake ya nyumbani, hili hapana”. Alisisitiza Prof. Maghembe.


Kwa mujibu wa Waziri Maghembe Bw. Mohammed Kilongo ambaye Idara yake ndiyo inatoa vitabu kwa ajili ya kukusanya maduhuri ya Serikali katika Mikoa yote na Wilaya zote nchini analazimika kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi ambapo ukikamilika sheria itachukua mkondo wake bila uonevu wowote.


Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Maliasili na Utalii amewaagiza pia Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) kutumia muda wa siku saba kurudi katika jengo la Wizara ya Maliasili na Utalii maarufu kama Mpingo House ambalo walihama mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka jana na kwenda kupanga katika jengo la NSSF Mafao House lililopo Ilala.


“Wakati tunajenga nyumba hii hapa, tumejenga jengo hili ni kama jengo la misitu ndio maana linaitwa Mpingo House kwa maana ni jengo la Misitu, ninyi wenyewe mmejenga jengo kubwa hili mmemaliza mmehama, Naagiza jumatatu Januari 11 muwe mmesharudi katika jengo hili, ghorofa ya tatu nikija kukagua niwakute, haiwezekani mueleze matatizo yote mliyonayo muhame nyumba ya Serikali mkapange jengo hapo jirani” Alisema Prof. Maghembe.


Katika hatua nyingine ya kuboresha uhifadhi wa Misitu nchini Waziri Maghembe ameiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili kuhakikisha inajiimarisha katika lengo lake kuu la uhifadhi kwa kushirikiana na wadau wanaohusika kuhakikisha Mamlaka iliyolengwa ya Uhifadhi Misitu inakamilika.


“Tunataka tutoke kwenye Wakala wa Huduma za Misitu (Tanzania Forestry Services Agency) twende kwenye Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu (Tanzania Forestry Services Authority) ili tuweze kufanya vizuri zaidi kwenye eneo la uhifadhi na uendelezaji wa misitu nchini, Katibu Mkuu tunaomba pia usaidie kufanikisha hili” Alisema Prof Maghembe.


Aliongeza kuwa wakati wa kuundwa Mamlaka hiyo ni vizuri pia Idara ya Misitu na Nyuki ya Wizara ya Maliasili ikatenganishwa na kila moja kuwa Idara kamili kutokana na umuhimu wa kila sekta katika kujenga uchumi wa nchi kwa kutoa fursa ya kuboresha maeneo hayo na kuongeza pato la taifa.


Ameitaka pia Idara ya Misitu na nyuki kupitia Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kuhakikisha kuwa inaongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya yote ya ubadhilifu pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato na kuboresha vyanzo vilivyopo.


Akizungumzia mchango wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) kwenye pato la taifa Mtendaji Mkuu, Bw. Juma Mgoo amesema katika mwaka huu wa fedha TFS imeweka makisio ya kukusanya Tsh. Bilioni 88 ambapo mpaka hivi sasa wameshakusanya zaidi ya asilimia 20 na makisio hayo.


Waziri Maghembe akizungumzia kuhusu uvamizi kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba amewataka wananchi wote waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa kwa ajili ya kuchunga mifugo waondoke ndani ya siku saba zijazo, na wale walivamia mapori ya akiba kwa shughuli za kilimo na ufugaji waondoke ndani ya miezi mitatu ijayo.


"Serikali itawaondoa kwa nguvu wasipotekeleza agizo hili la kuondoka katika maeneo ya hifadhi za taifa na kwenye mapori ya akiba yaliyohifadhiwa” Alisisitiza Prof. Maghembe.


Akizungumzia kuhusu biashara ya Mkaa, Prof. Maghembe amewaagiza wataalamu wa Idara ya Misitu kusimamia biashara ya mkaa kwa kuzingatia taratibu na sheria ikiwa ni pamoja na kuzuia usafirishaji wa Mkaa nje ya nchi.


Ameongeza kuwa nishati ya Mkaa ni muhimu lakini Tanzania ina hifadhi kubwa ya makaa ya mawe ambapo ameitaka Idara ya Misitu kwa kushirikiana na wadau wengine kuona ni namna gani ya kuweza kutumia mbadala huo kwa kuzalisha makaa hayo ya mawe kwa matumizi ya kawaida ili kuokoa misitu nchini.


Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri yatafanyiwa kazi kwakuwa lengo lake ni kuona dhamira ya msingi ya Serikali ya awamu ya tano inafikiwa ya kubana matumizi, kuongeza mapato ya Serikali na kuhifadhi maliasili za taifa ikiwemo misitu.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ,
Wizara ya Maliasili na Utalii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527