MAHAKAMA KUU YAPIGA STOP BOMOA BOMOA DAR


Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi imeweka zuio la kubomoa nyumba zilizopo katika wilaya ya Kinondoni hasa zile ambazo wamiliki wake wameleta ombi lao mahakamani kuzuia kubomolea.


Akitoa hukumu hiyo jana mbele ya walalamikaji, wakili wa Serikali, mawakili wa walalamikaji na wananchi, Jaji wa Mahakama hiyo kuu ya Ardhi Mhe.Panterine Kente alisema kuwa mahakama imezingatia maelezo toka pande zote mbili kwa kuangalia madhara watakayopata wananchi kwa kutekelezwa kwa zoezi hilo.


Jaji Panterine Kente aliongeza kuwa mahakama ya Ardhi haijaweka zuio la bomoa bomoa kwa Tanzania nzima bali kwa wale tu walioleta maombi ya shauri la zuio la kubomolewa nyumba zao na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea na uwekaji wa alama za x na ubomoaji wa nyumba zilizopo sehemu hatarishi na sehemu zisizostahili.


“ Nakuagiza Wakili Abubakari Salim uniletee majina yote leo hii na sio kesho ya waliofungua shauri la zuio la kutobomolewa nyumba zao ili tuweze kuendelea na zoezi la ubomoaji” Alisema Jaji Kente


Akizungumza baada ya kutolewa hukumu hiyo Wakili wa Serikali Manchare Henche alisema wamepokea hukumu hiyo na wao wataendelea na majukumu yao ya ubomoaji wa maeneo hatarishi kama Mahakama ilivyoeleza kuwa haijatoa zuio la bomo bomoa kwa Tanzania nzima ila kwa wale tu walioleta shauri la zuio.


“Tunaomba walio maeneo ya mabondeni wahame kwani zoezi hili linaendelea na zoezi la uwekaji wa alama za x litaendelea kama kawaida kwa maeneo mengine nje ya haya yaliyowekewa zuio” Alisema Henche.


Aidha akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutolewa hukumu hiyo Mbunge wa Jimbo la Kinondoni Maulid Mtulia alisema kuwa uamuzi umeridhisha na pia mahakama imetenda haki kwa wananchi wa kinondoni na wanashukuru kwa kupata nafasi ya kusikilizwa kwa hoja zao.


Kesi hiyo namba 822 ilifunguliwa na wawakilishi nane wanaowawakilisha wananchi 674 ambao nyumba zao zilikuwa katika mpango wa kubomolewa chini ya sheria za mipango miji.

Baada ya Mahakama kuu ya Tanzania kitengo cha Ardhi kutoa zuio la bomoa bomoa kwa wakazi hao kesi ya msingi itatajwa tena Januari 11.

Mkuu wa Mkoa Wa Dar Atoa Tamko

Wakati mahakama kuu ikisimamisha zoezi la bomoa bomoa, Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Said Meck Sadick amejitetea na kukanusha taarifa za upotoshaji ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa kisiasa hususani wenyekiti wa mitaa na baadhi ya wakazi wanaoishi maeneo hatarishi ya mabondeni juu ya serikali kuvunja nyumba, ikizingatia kutotoa maeneo mbadala ya kujenga makazi mapya ya kudumu.




Meck sadick amesema mwaka 2011 yalipotokea mafuriko serikali iliwapatia viwanja wakazi waliokuwa na nyumba katika maeneo hatarishi ya mabondeni kwa Wilaya zote tatu za Mkoa Dar es Salaam katika eneo la Mabwepande wilaya Kinondoni.




Kwa mujibu mkuu wa mkoa jumla ya viwanja 1007 viligawiwa kwa wakazi hao wa mabondeni na viwanja vitatu havikugawiwa kwa sababu viliangukia maeneo yasiyofaa kwa makazi.




Aidha sambamba na kupatiwa viwanja wakazi hao walipatiwa misaada ya kibinadamu pamoja na vifaa vya kiujenzi ikiwemo mifuko ya saruji 100 mabati na mbao kila kaya na kuwawekea huduma muhimu za kijamii.




Amesema wakazi hao wamediriki kuuza viwanja vyao kwa bei ya chini na kurudi maeneo waliyokuwa wakiishi awali na wengine kuuza na kupangisha nyumba zao walizojenga mabondeni licha ya Serikali kuwataka waondoke katika maeneo hayo hatarishi.




Vile vile amesema Serikali kwa kushirikiana na halmashauri zote nchini imeanza na inaendelea na zoezi la bomoa bomoa kwa ajili ya kuwaondoa wakazi wote wanaoishi maeneo hatarishi na wale waliovamia maeneo yasiyostahili kujengwa.




Pia amesema zoezi hili la bomoa bomoa litafanyika nchi nzima ambapo kwa sasa limeanzia Mkoa Dar es Salaam na wakazi waliojenga katika maeneo hatarishi wabomoe wenyewe na kuondosha baadhi ya vifaa vya ujenzi ambavyo vitawasaidia kwenda kuendeleza makazi mapya katika viwanja walivyopewa na serikali.




Amewataka wananchi kuacha kuendelea kulalamika wakati wanafahamu kuwa wamevunja sheria licha ya serikali kuwataka kuondoka kabla hawajapata madhara ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527