LOWASSA AVUNJA UKIMYA..AWAPA ONYO WATENDAJI WA SERIKALI WANAOWAANDAMA WALIOKUWA WANAMUUNGA MKONO KWENYE UCHAGUZI





Aliyekuwa mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda UKAWA Mh.Edward Lowassa amelalamikia baadhi ya watendaji wa serikali kwa kuwaandama na kuwatisha wananchi na wafanyabiashara waliokuwa wanaunga mkono vyama vya upinzani na amezitaka idara zinazohusika kuchukua hatua ili kuepusha matatizo yasiyo ya lazima.



Akizungumza katika ibada maalum ya kukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika kanisa la kilutheri wilayani Monduli Mh Lowassa amesema amepokea malalamiko ya kuwepo kwa uonevu na vitisho kwa wadau walioonekana kuunga mkono vyama vya upinzani licha ya kuwa ni haki yao kikatiba. 


Pia Mh Lowassa aliyekuwa mbunge wa jimbo la Monduli kwa tiketi ya (CCM) kabla ya kuhamia Chadema na kuwa mgombea urais amesema ataendelea kusaidiana na mbunge wa sasa Mh Julias Kalanga (Chadema) kutatua kero za wananchi na kuhakikisha kuwa misingi aliyoijenga inakuwa endelevu. 


Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa dini na wananchi waliohudhuria ibada hiyo wamepongeza uvumilivu wa kisiasa ulioonyeshwa na Mh Lowassa ambao umeendelea kuimarisha amani na utulivu nchini na wamewaomba wanasiasa wengine kuiga mfano huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527