
Mmoja wa wahanga hao akiwa katika hospitali ya wilaya ya Kahama.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida watu 5 kati ya 6 waliokuwa wamefunikwa na kifusi cha udongo kwa siku 41 katika machimbo madogo wa Nyangalata wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameokolewa wakiwa hai.
Wakizungumza katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama ambako wamelazwa kwa matibabu ,walikuwa wakiishi kwa kula wadudu kama vile vyura,mende magome ya miti hali iliyowasababisha kuendelea kuwa hai kwa siku 41 hadi jana jioni walipookolewa.
Kwa mujibu wa wachimbaji hao, walikuwa wakitumia kofia zao kukinga maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu kwa ajili ya kunywa.
Wahanga hao ni Onyiwa Kanyimbo(55),Msafiri Jerald(38) Amosi Muhangwa(25), Chacha wambura(53) na Joseph Burule(44) na aliyefariki dunia ni Mussa Supana.
Inaelezwa kuwa wachimbaji hao walifukiwa Oktoba 5, mwaka huu saa 5.00 asubuhi wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji chini ya ardhi.
Watu walioshuhudia tukio hilo, walisema ardhi ya juu ya machimbo hayo ilititia na kuporomoka kutokana na mvua iliyonyesha, na hivyo kuwafunika wachimbaji hao.
Wakati huo jitihada za uokoaji zilifanikisha kuokolewa wachimbaji sita wakati wengine hawakuweza kufikiwa, ikizingatiwa pia kuwa zilikosekana taarifa sahihi za idadi yao na eneo halisi walikokuwa wamefukiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema wachimbaji hao waliokolewa baada ya kugunduliwa na wazamiaji walioingia kwenye mashimo hayo kwa lengo la kuiba mchanga.
Alisema wachimbaji hao walisikia watu wakiomba msaada katika mashimo hayo.
“Baada ya wachimbaji hao kusikia sauti, waliwasiliana na wenzao na kuanzisha jitihada za kuwaokoa,” alisema.
Kamanda Kamugisha alisema hatimaye waliweza kuwatoa katika mashimo hayo jana wakiwa wamekaa kwa siku 41 tangu Oktoba 5, mwaka huu.
Alisema mchimbaji mmoja, Musa Spana, alikufa siku chache baada ya kufukiwa na kifusi kwa kukosa chakula.
Mmoja wa wachimbaji hao, Wambura, alisema awali walifukiwa sita, lakini bahati mbaya mwenzao Spana alifariki dunia siku chache baadaye baada ya kukataa kula mizizi.
Alisema hatua hiyo ilisababisha akumbwe na ugonjwa wa kuhara uliosababisha kifo chake.
“Tulikuwa tukitumia miti inayojengea kingo za mashimo kama chakula pamoja na wadudu wadogo wadogo ndani ya mashimo hayo, hasa mende.
“Pia tulikuwa tukitumia kofia zetu ngumu (helmet) kukinga maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu ya ardhi ingawa yalikuwa ni machafu.
“Mwenzetu Musa alifariki dunia baada ya kukataa kutumia vitu hivyo,” alisema Wambura.
Akizungumzia tukio hilo, Naibu Kamishna wa Madini, Ali Samaje, aliwataka wachimbaji wadogo kuimarisha migodi yao huku wakizingatia masuala ya usalama zaidi.
Samaje alisema hatua hiyo itawafanya kufanya kazi zao kwa uhakika na kuepukana na ajali kama hizo.
Pia aliwataka kuacha kuchimba madini kwa ajili ya kuuza tu, bali wajaribu kusaidiana katika mambo mbalimbali wanapokuwa na matatizo.
Alitoa ushauri huo kwa kuzingatia kuwa shughuli zao wanaziendesha katika maeneo ambayo hayako salama.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Joseph Ngowi, alisema ameshtushwa na tukio hilo la wachimbaji hao kukaa kwa muda huo shimoni.
Alisema tukio hilo linaweza kuwa ni maajabu ya nane ya dunia.
Dk. Ngowi alisema kwa sasa waathirika hao wanapatiwa matibabu ya saikolojia pamoja na lishe maalumu kuhakikisha wanarudi katika hali zao za kawaida kwa muda usiopungua siku saba.
“Waathirika hao tunao katika hospitali yetu katika kitengo cha lishe.
“Kwa sasa hawaoni hadi zipite siku saba kwa sababu walikaa gizani muda mrefu.
“Pia tunawapatia matibabu ya saikolojia kuhakikisha wanakuwa sawa na afya ya akili,” alisema.
Wakati huohuo, Wizara ya Nishati na Madini imesema juhudi za kutafuta mwili wa Musa zinaendelea.
Taarifa hiyo ilitolewa na Msemaji wa Wizara hiyo, Badra Mosoud, Dar es Salaam leo.
Alisema Musa alifariki dunia siku 15 zilizopita.
“Wachimbaji hao walikuwa wakiishi umbali wa mita 100 kutoka juu ya ardhi, huku wakila magome ya miti na matone ya maji yaliyokuwa yakidondoka ambayo waliyakinga kwa kofia zao,” alisema.
Alisema wachimbaji hao walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama juzi wakiwa na hali mbaya.
Badra alisema hivi sasa wanaendelea vizuri na matibabu, huku wakipatiwa lishe ili kurejesha afya zao.
Alitoa wito kwa wachimbaji wote kutumia vifaa vya kisasa katika uchimbaji wao ili kupunguza maafa.
Meneja wa mgodi mdogo huo Amos Mbanga amesema timu ya mafundi ilifanya utafiti na kugundua kuna sauti za watu zikiita na kuamua kupeleka waokoaji kwa kushirikiana na serikali pamoja kampuni ya Acacia na kufanya uokoaji huo kuchukua masaa 24.
Kwa upande wake katibu mkuu wa wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Shinyanga Bw. George Kibusy ametoa rai kwa yeyote atakayeguswa kutoa masaada wa hali na mali kwakuwa wahanga hao wana mahitaji makubwa ikiwemo nguo na chakula.
Ni jambo ambalo sio rahisi kuingia akilini na kueleweka binadamu kukaa chini ya ardhi kwa zaidi ya siku arobaini lakini watu hawa watano walijikuta wakiishi kwa kudura za mwenyezi mungu.
Social Plugin