Duh!! WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AGOMA KUGOMBEA UBUNGE TANZANIA




WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amekataa ombi la wananchi wa jimbo lake la uchaguzi la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo aliyoianzisha.



Akizungumza baada ya Ibada ya Jumapili katika kigango cha Kanisa Katoliki cha Kibaoni wilayani Mlele (Jumapili, Julai 19, 2015), Waziri Mkuu Pinda amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa yeye kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa jimbo la Katavi.


Amesema yeye ataendelea kuwa karibu na wananchi wa Katavi wakati wote na kwa vile atakuwa na muda wa kutosha atashiriki kikamilifu katika mikakati mbalimbali ya kuwaletea maendeleo wananchi ili waweze kujikwamua kutoka kwenye umaskini.

Mheshimiwa Pinda aliwaasa wananchi wa jimbo la Katavi wawe makini katika kuchagua mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao.


Akimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani Mlele, Padri Aloyce Nchimbi aliwaasa wananchi wa Wilaya ya Mlele kumuenzi Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hata atakapokuwa amestaafu kwani bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea maendeleo.


Waziri Mkuu yuko kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele kwa ajili ya mapumziko mafupi.


Leo saa 10 jioni ndiyo mwisho wa kurejesha fomu za ubunge ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).


IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 19, 2015.

Chanzo- Mtetezi wa Haki blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post