MSIBA WA MBUNGE WA GEITA DONALD MAX WALETA BALAA, WANANCHI WADAI MBUNGE HAJAFARIKI, MWENYEKITI WA CCM ASEMA "MAITI SIYO YA CCM"

  Rais Jakaya Kikwete, mkewe Mama Salma, wakitoa heshima za mwisho mbele ya Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Geita, marehemu Donald Kelvin Max, wakati wa shughuli za kuaga mwili zilizofanyika  Juni 27, 2015 kwenye Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam

Sakata la Mbunge wa jimbo la Geita Marehemu Donald Kelvin Max kuzikwa jijini Dar Es Salaam pasipo wananchi wake kupata fursa ya kuaga mwili wake limechukua sura mpya baada ya baadhi ya wakazi wa jimbo la Geita Wilayani Geita,wakiwemo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kukana kufiwa na mbunge wao kwa kile walichodai alikuwa mwakilishi wa eneo alikozikwa huku chama cha mapinduzi mkoa wa Geita kikidai hakuna kanuni zinazolazimisha mbunge kuzikwa kwenye jimbo lake.



Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Malunde1 blog,ikiwa ni siku moja tangu mbunge wao kuzikwa,baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wananchi  huku wakionekana kukerwa na jambo hilo walidai kuwa,wanachojua mbunge wao yuko hai na iwapo angekuwa amefariki dunia angeletwa Geita kuagwa na wananchi wake.

Neema Steven Chozaile  mwenyekiti wa BAVICHA Mkoa wa Geita alidai kuwa,kitendo kilichofanywa na chama cha mapinduzi cha kuruhusu mbunge wa Geita kuzikwa kimya kimya jijini Dar kimewafumbua macho wananchi na kwamba safari hii hawatafanya makosa katika kuchagua mwakilishi wao.

‘’Tumepata fundisho kwamba tunapochagua mtu tuwe makini,tunayemtambua alipozaliwa,ni mtoto wa Fulani maana haiwezekani mbunge wa Geita asiletwe hapa akaagwa na waliomchagua tena kwa kura nyingi,kama CCM wanaruka na helkopita kuhudhuria sherehe za mtia nia Monduli walishindwa kutumia usafiri huo kuleta maiti ya mbunge wetu akaagwa hapa kisha wakamzika watakapo,ndiyo maana tunasema huyo hakuwa mbunge wetu bali wa Dar alikozikwa’’alisema.

 ‘’Mwaka 2010 niliamka alfajiri  kwa ajili ya kuwahi foleni ili nimchague mbunge wangu Max,nikafanikiwa..nilivyosikia kwamba amekufa sikuamini ikanibidi nianze kutafuta msiba ulipo hadi mtaa wa Katoma wanakodai ni nyumbani kwake’’

‘’Lakini hakukuwa na dalili za msiba zaidi ya mikusanyiko ya wanaojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR,lakini wakati nikiendelea kuhangaika nijue msiba ulipo ndiyo nilipoelezwa msiba uko Dar na atazikwa huko..hii imetudhalilisha sana wakazi wa Geita’’alisema Fidelis Kanani mkazi wa Nyerere Road.

Zephania Mussa ambaye ni mkazi wa mtaa wa Nyanza Kalangalala mjini Geita,alisema ‘’Sisi Geita walishatudharau maana watu wa kuja ndiyo wanachukuwa uongozi,mfano marehemu Max alitudanganya ni mkazi wa Geita,tutamchagua tena nkwa kishindo tukiamini ni mwenzetu’’

‘’Kitendo cha mbunge wetu kuzikwa nje ya hapa na bila kuagwa na waliomchagua kimetuuma sana na huu ndiyo mwisho kwa wanaGeita kuendelea kuwa shamba la bibi,kwa sasa mtu atakayekuja kutuomba ridhaa ya kutuongoza tutamtaka atupeleke nyumbani kwao,tujuwe ukoo wake na mpaka alipozikwa babu yake maana tulkijipanga tumzike mbunge wetu kwa heshima zote kumbe anazikwa Dar imeumiza sana nasoi tunasema waliomzika ndiyo waliomchagua wetu hajafa bado’’alisema Mussa.

 ‘’Sisi kam wanageita hili jambo limetuchanganya na ndiyo maana tunasema hatujafiwa na mbunge wafiwa ni wakazi wa Dar,haiwezekani mtu tuliyemwamini kama mwakilishi wetu azikwe kimyakimya sisi tuliopigwa mabomu ajili yake tusimuage na kwa nini azikwe huko,inamaana alitudanganya ni mkazi wa Geita ili hali sivyo?’’alihoji Lucas Charles mkazi wa mtaa wa Moringe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita Kamanda Alphonce Mawazo akitoa maoni yake alisema‘’Maoni yangu ni kwamba tumehadaiwa,mimi nilitoka mbeya kumzika mbunge wangu nikiwa sina shaka atazikwa Geita,kumbe tulichagua tulichagua mtalii na ndiyo maana alitelekeza jimbo kwa muda mrefu akiwa hajaanza kuugua maradhi yanayomsumbua’’

‘’Mbunge ni lazima awe na uhusiano wa ardhi ya pale anapowakilisha,awe na wajomba,dada,shangazi,babu zake, watu aliocheza nao utotoni,aliosoma nao,angalu awe anaguswa na damu ya pale,lakini  sisi wana Geita tulichagua kwa ushabiki na hatukujua kwamba tulichagua mtalii’’

‘’Msiba huu umetufumbua macho na umetufundisha mambo mengi  kwamba inatubidi tutambue kwamba Ubunge ni Uchifu na Chifu hawezi kutoka eneo jingine,lazima atoke eneo lilelile alilozaliwa maana kama mimi nilitegemea niwape pole ndugu zake,mama,mke wake na ndiyo maana nikatoka Mbeya kuwahi mazishi harafu nikakuta hata harufu ya msiba hakuna’’

‘’Kwa kweli wana Geita tumejisikia vibaya na sisi wananchi tujifunzekwani  na maendeleo hayaji kwa kuchagua mtu asiye mkazi,kwani angekuwa mkazi ningempa mkono wa pole  shangazi yake lakini hakuwepo,nimekuja Dar napo sikufanikiwa maana sikujua hata msiba uko wapi’’alisema Mawazo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita,Joseph Kasheku Musukuma alipotakiwa kuzungumzia hali hiyo alidai kuwa,maiti ni ya familia ya Max na hakuna kanuni kwenye chama chao cha Mapinduzi(CCM)zinazowalazimishwa azikwe eneo alilokuwa akiliwakilisha kama Mbunge.

‘’Anayehoji kwa nini Mbunge wao hakuzikwa Geita,mwambie kuwa maiti siyo ya ccm ni ya familia ambayo ndiyo ilitoa ratiba ya wapi azikwe,mi sidhani kama kuna sababu ya yeye kuzikwa Geita wakati kwao ni Dar es Salaam na ndugu zake wengine wamezikwa huko,kama wanasema walimchagua kwa kishindo na wanashangaa kuona hakuzikwa Geita waulize wakati anaumwa nani aliyekwenda kumsalimia kwa kishindo?’’alisema Musukuma

Mbunge Max alifariki juni 23  katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi(ICU)kwa zaidi ya mwaka mmoja akisumbuliwa na kansa ya Ubongo kwa zaidi ya miaka mitatu ambapo alipatiwa matibabu nchini India kabla ya kurudishwa hapa nchini. Alikuwa mbunge wa jimbo la Geita tangu mwaka 2010 hadi mauti yanamkuta na amezikwa juni 27,2015 makaburi ya Kinondoni jijini Dar Es Salaam.

Na Victor Bariety-Malunde1 blog Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527