Hii Imekaa POA!! WANAUME LAKI TATU WATAHIRIWA BURE SHINYANGA NA SIMIYU!!


Wakazi wa Shinyanga wakiwa nje ya banda la shirika la Intrahealth International  katika viwanja vya Shycom mjini Shinyanga ambapo kunafanyika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani,kitaifa mkoani Shinyanga,wakisubiri kupima afya zao ili kujua kama wameambukizwa VVU ama la,banda hilo linatoa huduma ya tohara kwa wanaume,ambapo huduma hiyo itaendelea hadi Mei 16,mwaka huu ili kuwapa fursa wakazi wa Shinyanga ambao hawajafanyiwa tohara
Nje ya banda hilo

Wakazi wa Shinyanga wakisubiri huduma nje ya banda la shirika la Intrahealth international

Zaidi ya wanaume 315,000 wamefanyiwa tohara ya wanaume kwa ajili ya kujikinga na Virusi vya UKIMWI katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na wilaya ya Rorya mkoani Mara ikiwa ni sawa na asilimia 39 ya wanaume wanaoishi katika mikoa hiyo miwili na wilaya ya Rorya.

Haya yamebainishwa jana na mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe baada ya Malunde1 blog kutembelea banda la shirika la Intrahealth International wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya Wauguzi duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Shinyanga.

Dkt Kapologwe alisema huduma ya tohara imekuwa ikitolewa na watumishi wa idara ya afya waliopewa mafunzo maalumu na kati ya wahudumu hao wamo wauguzi.

Dkt Kapologwe alisema idadi hiyo ya wanaume waliotahiriwa imepatikana tangu serikali kwa kushirikiana na Intrahealth International kuanza kutoa huduma ya tohara ya mwanaume kwa ajili kujikinga na VVU mwaka 2011.

“Wauguzi wametoa mchango mkubwa sana katika kufanikisha kampeni ya kitaifa ya tohara ya mwanaume kwa ajili ya kujikinga na UKIMWI,” alisema mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dr. Ntuli Kapologwe.

Kwa mujibu wa  Dr. Kapologwe wauguzi wanawakilisha zaidi ya asilimia 55 ya watumishi wote wa idara ya afya, hivyo uwepo wao ni msaada mkubwa kutatua changamoto za utoaji huduma ya afya.

“Kwa kuwapa mafunzo ya utoaji wa huduma ambazo kitaaluma si kazi yao tumeweza kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo na vituo ambako kada kama famasia ama madaktari hawapo,” alisema Dkt. Kapologwe.

Kwa upande wake mratibu wa huduma za UKIMWI mkoani Shinyinga Dkt. Mawazo Amri alisema Kutokana ufadhili toka serikali ya marekani kupitia mfuko wa rais wa marekani wa kudhibiti UKIMWI (PEPFAR) idara ya Marekani ya Tiba na Udhibiti wa Maradhi (CDC) huduma ya tohara imeweza kufikishwa hadi kwenye maeneo ya vijijini ambako kwa kawaida hakuna wahudumu wa afya wa kutosha wenye ujuzi wa kufanya tohara.

“Kupitia kamati ya afya ya mkoa na kamati za afya za kila wilaya na IntraHealth tunasambaza huduma ya tohara kwenye vituo vya afya vya pembezoni na hivyo kuhakikisha kuwa kila  mwanaume ambaye anaihitaji huduma hii anaipata, alisema Dkt  Amri.

Alisema serikali ya Tanzania ilianzisha kampeni ya kufanya tohara ya mwanaume kwa jamii ambako hazikuwa na mila ya tohara baada ya kuthibitika kisayansi kuwa tohara ya mwanaume inapunguza kwa asilimia 60 uwezekano wa mwanaume aliiyefanyiwa tohara kuambukizwa VVU.

Dkt Amri alisema tohara ya mwanaume, zaidi ya kuongeza usafi, pia inachangia kupunguza uwezekano wa mwanamke ambaye mwenzi wake ametahiriwa kupata saratani ya shingo ya uzazi.

Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa yenye ushamiri mkubwa wa maaumbikizi ya UKIMWI na idadi ndogo ya wanaume ambao wamefanyiwa tohara, kwa mujibu wa takwimu za  viashiria vya malaria na UKIMWI  za mwaka 2011/2012.

Mikoa mingine ambayo imekuwa ikifanya jitihada kusambaza huduma ya tohara ya mwanaume ni Njombe, Geita, Mbeya na Rukwa.

Idadi ya wanaume waliokwisha fanyiwa tohara inakaribia nusu ya idadi ya wanaume wanaoishi katika mkoa wa Shinyanga na Simiyu.

Huduma ya tohara ya mwanaume inatolewa kwa aushirikiano kati ya serikali ya Tanzania kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii na wanau wa maendeleo yaani shirika la Intrahealth International ambalo hufanya program mbalimbali za afya zenye kuweka mbele utendaji wa wafanyakazi wa idara ya afya.

Siku ya wauguzi kitaifa  inaadhimishwa kitaifa mjini Shinyanga ikiwa na kauli mbiu isemayo wauguzi kiini cha mabadiliko; huduma bora za afya kwa gharama nafuu ambapo kilele chake ni leo Mei 12,2015 lakini huduma ya tohara itaendelea kutolewa hadi Mei 16 mwaka huu katika viwanja vya Shycom.
Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post