Noma Sana!! MAJI YAADIMIKA ZAIDI YA WIKI MOJA SASA MJINI SHINYANGA


Wakazi wa manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga wamezilalamikia zinazozalisha maji katika manispaa hiyo kutokana na maji kukatwa kwa zaidi ya siku tano bila taarifa yoyote hali inayowakwamisha kufanya kazi zo za maendeleo.
Wakizungumza na Malunde1 blog kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamezitupia lawama mamlaka zinazo zalisha na kusambaza maji Shinyanga (Shuwasa) na (Kashwasa), kwa kushindwa kutatua tatizo hilo la maji mapema na kuwaacha wateja wao wakiendelea kutaabika kwa kukosa maji.


Walisema tatizo hilo la uhaba wa maji limekuwa kero kwao, hali ambayo imekuwa ikiwamisha  kufanya shughuli zao za maendeleo na kupoteza muda mwingi wakitafuta maji pembezoni mwa mji, na wakati mwingine kulazimika kutumia maji ya visima vya maji ambavyo havina usalama.


“Tunasikia tu kuna hitilafu ya umeme,tunasikitika kwa kukosa maji zaidi ya siku tano, ankara za maji tunalipa kwa wakati, lakini huduma tunayopewa na mamlaka hizi ni mbovu, tena wanakata maji bila taarifa na hatujui tatizo linalosababisha tukose huduma ya maji, na kutufanya tuishi kwa shida” alieleza Halima Maganga mkazi wa Ndala.

“Hivi sasa tunalazimika kununua dumu la lita 20 shilingi 800/= au 1000/=,na wakati mwingine tunalazimika kutumia maji ya madimbwi au visima,maji ambayo kimsingi sio salama”,aliongeza Tungu Manyongo mkazi wa Bugayambelele.

Akizungumzia malalamiko hayo mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Safi na usafi wa Mazingira manispaa ya Shinyanga (SHUWASA), Sylivester Mahole, ambao ndiyo wanasambaza maji mjini Shinyanga, alisema tatizo hilo la ukosefu wa maji limetokana na mitambo ya mamlaka ya usambazaji maji katika miji ya Shinyanga na Kahama (KASHUWASA) kuharibika na kushindwa kuzalisha maji.


Mahole alisema baada ya kupa taarifa za kuharibika kwa mitambo  ya kuzalishia maji kutoka kwa wenzao (KASHUWASA), ndipo walipoamua tarehe 8,mwezi huu kuanza kutumia vyanzo vyake vya zamani vya bwawa la Ning’wa kusambaza maji mjini humo, ambayo hata hivyo nayo hayakidhi mahitaji ya wakazi hao.


Aidha kwa upande wake mkurugenzi wa mamlaka ya usambazaji wa maji kwa Miji ya Shinyanga na Kahama (KASHUWASA) Clement Kivegaro ambao wanazalisha maji hayo ya ziwa Victoria na kuwauzia (SHUWASA), alikiri kuwepo kwa tatizo kwenye mitambo hiyo ya kuzalisha maji.
Alisema hali hiyo imetokana na hitilafu ya umeme na hivyo mitambo hiyo kukosa nguvu ya kuzalisha na kusukuma maji.


Hata hivyo Kivegaro alisema tatizo hilo hivi sasa lipo kwenye matengenezo huku wakishirikiana na Shirika la umeme Tanesco, kwa ajiri ya kupata ufumbuzi wake ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi na salama kama kawaida, huku akibainisha kuwa hajui lini suluhu yake itapatikana .
Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post