Makubwa ya Geita!! MTENDAJI WA KATA ACHEZEA KICHAPO HADI KULAZWA HOSPITALI KISA KAGOMA KUTOA RUSHWA KWA MRATIBU WA TASAF

Diwani wa kata ya kamwanga Dionizi Bugali akimsaidia kumnyanyua mtendaji wa kata yake Sabini Ndaki anayedaiwa kupigwa  na mratibu wa Tasaf wilaya  Geita baada ya kumnyima Rushwa ya shilingi laki tano-picha na Valence Robert-Malunde1 blog Geita.


Muuguzi wa Hospitali wilaya ya Geita Zaituni Hussein akimuhudumia mtendaji wa kata ya Kamwanga  jana anayedaiwa kupigwa na msimamizi wa kata ambaye pia ni mratibu wa Tasfu Wilaya ya Geita Damiani Aloyce-picha na Valence Robert-Malunde1 blog Geita.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida afisa mtendaji wa kata ya  Kamwanga Sabini Ndaki amechezea kichapo kikali kutoka kwa mratibu wa TASAF wilaya ya Geita Mkoani Geita Damiani Aloyce kwa maelezo kuwa amenyima fedha za kumsainia muhtasari

Tukio hilo la aina yake lilitokea jana katika ofisi za TASAF Mjini Geita, saa 9:00 alasiri, ambapo mtendaji huyo alikwenda kwa mratibu huyo ambaye pia ni mlezi wa kata hiyo, ili amsainie muhtasari wa  vifaa vya ujenzi wa maabara katika kata ya Kamwanga ambapo alimwomba Shilingi laki tano ili amsainie.

Akizungumza kwa shida kwenye wodi namba tano katika hospitali ya wilaya ya Geita Ndaki alisema kuwa alifika kwenye ofisi za Tasaf kwa lengo la kusainiwa muhtasari uliopitishwa kwenye kikao cha kata kwa ajili ya vifaa vya ujenzi wa maabara.

“Nimeshambuliwa kwa kipigo na mratibu kwa kosa la kumnyima sh. Laki tano alizoniomba ili asaini  muhtasari niliompelekea ili nikachukue vifaa vya ujenzi jambo ambalo nilikataa, kukataa hivyo alinifukuza huku akinisukuma  nikadondoka chini, akanyanyua kiti  na kunipiga, mkono wangu umepata majeraha na nina maumivu makali kwenye mwili wangu”alisema Ndaki.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Adamu Sijaona alithibitisha kumpokea majeruhi huyo na kwamba hali yake inaendelea vizuri .

Kwa upande wake Diwani wa Kamwanga Dionizi Bugali  kupitia CHADEMA alikiri kuwepo kwa tukio hilo la kupigwa mtendaji wake, ambapo alilaani kitendo hicho na alisema  jambo hilo ni la aibu na ametaka uchunguzi ufanyike haraka ili mhusika achukuliwe hatua kali za kisheria.

“Jambo hili limenisikitisha kweli kwanza ni kitendo cha aibu na haya mambo yamekuwa yakijitokeza ya watendaji kuombwa rushwa ili kupitisha miradi mbalimbali kwa hali hii hatuwezi kufika popote”alisema Bugali.

Waandishi wa habari walimtafuta Kaimu Mkurugenzi wa halimashauri ya wilaya Deusi Seif ili kutaka kujua kama suala hilo limefika kwenye ofisi yake, ambapo alisema hajapokea taarifa hiyo na kwamba atalifuatilia sakata hilo.

 Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post