KILICHOSEMWA NA MWENYEKITI WA ALAT SHINYANGA KUHUSU RAIS WA TANZANIA,MAGUFULI KUWA WAZIRI MKUU

Wakati mbio za urais zikiendelea kukolea,mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) mkoa wa Shinyanga Justine Sheka(Pichani) amewataka viongozi kutoka kanda ya ziwa waliotangaza nia ya kugombea urais waunganishe nguvu kwa Edward Lowassa huku akimtaka Lowassa kuchukua fomu mapema kwani historia inaonesha kuwa ndiyo kiongozi pekee wa kuitawala Tanzania katika kipindi hiki.



Sheka aliyasema hayo juzi mjini Shinyanga wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema Jumuiya ya serikali za mitaa mkoa wa Shinyanga inaamini kuwa Lowassa ndiye kiongozi atakayeweza kuivusha nchi ya Tanzania hapo ilipofikia.


Sheka ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,alisema watu wanaoendelea kumuwekea pingamizi Lowassa hawaitakii mema nchi kwani historia inaonesha kuwa watanzania wengi bado wanamwitaji hasa wakikumbuka kazi nzuri aliyoifanya yeye binafsi wakati akiwa waziri mkuu kwa muda mfupi ,katika harakati za ujenzi wa shule za sekondari za kata ambazo hadi sasa zipo.


“Mimi kwa kushirikiana na wenyeviti wote wa ALAT wa halmashauri zote za wilaya pamoja na wajumbe walioko katika wilaya wa mkutano mkuu wa taifa wa Chama Chama Mapinduzi,tunamtaka Lowassa akachukue fomu mapema na asiwekewe kipingamizi cha aina yoyote”,alieleza Sheka.


“Tunaomba katika kanda ya Ziwa Victoria wagombea wengine wamuunge mkono mzee Lowassa kwa sababu tunaona nafasi ya urais inamfaa na  kimsingi ndiyo chaguo la watu wengi na historia inaonesha kuwa anafaa kuiongoza Tanzania”,aliongeza Sheka.


Alisema ni vyema waliotangaza nia ya kugombea nafasi hiyo nyeti ya urais kuunganisha nguvu kwa Lowassa ili wakati wa kuunda serikali wapatikane viongozi wazuri wa kuingoza nchi ambayo sasa inapitia katika changamoto mbalimbali.


“Kuhusu John Magufuli kushawishiwa kuchukua fomu ya kugombea urais ni jambo jema ,tunaamini ni kiongozi mchapa kazi sana,kwa mawazo yetu tunadhani ni bora angeunganisha kwa Lowassa ili itakapofikia wakati wa kuunda serikali basi wamwangalizie nafasi ya uwaziri mkuu ili kufanya kazi za serikali ziendelee vizuri kwa jopo litakuwa zuri sana”,alieleza Sheka.
Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post